MWANDISHI: Anderson Leng'oko
Utangulizi:
Kwa watu waliobahatika kulisoma somo hili katika sehemu yake ya kwanza watakumbuka kuwa tuliahidi kuangalia sababu za watu kuwa wazinifu. Roho Mtakatifu ametusaidia kutuletea baadhi ya sababu hizo katika sehemu hii ambapo zipo sababu za kiroho na za kimwili zilizochambuliwa zote kwa pamoja. Kama hujasoma sehemu ya kwanza ya somo hili nakushauri uisome kwanza sehemu hiyo ya kwanza HAPA ili upate mtiririko mzuri. Naamini Mungu atakuwa nawe unapoendelea kujifunza nasi sehemu hii ya ujumbe aliotupatia kwa neema yake.
KWANINI WATU WANAZINI/WANAKUWA WAZINIFU?
KUTOKUITAMBUA KWELI
Hii ndiyo sababu kuu ambapo nyingine zote zinazofuata zinajikita katika hii. Watu wengi wamejikuta wanakuwa wahanga wa dhambi hii ya zinaa kwa sababu hawaitambui kweli, kweli inayoongelewa hapa ni kweli ya Mungu. Hawajui kuwa Mungu aliyewaumba anachukia zinaa na wao kama wanadamu wanatakiwa kumheshimu Mungu kuliko kitu chochote kile. Hawajui kuwa wao ni hekalu la Mungu na kwamba mtu akiliharibu hekalu la Mungu ataharibiwa. Kutokujua ninakoongelea hapa ni hata kwa wale ambao wanaifahamu ile kweli, lakini hawaizingatii, hao bado hawajui hasa uzito na ubaya na hatari ya hicho wanachokifanya.
1Wakorintho 3:16-17Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?
Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.
Watu hawa hawaifahamu kweli hii, na wamefuata tamaa za miili yao wakiisha kudanganyika na kuzisikiliza tamaa zao bila kujua kuwa wanajipatia hukumu iliyo kubwa zaidi. Lakini ukitafakari na kuchunguza athari za mambo wayafanyayo, unakuja kuona kuwa watu hawa hawakujua wayafanyayo yana athari gani katika roho. Watu wengi hawaelewi thamani ya miili yao, thamani ya nafsi na thamani ya roho zao na wanaona kila kitu ni sawa tu. Hadi wanafikia hatua ya kujiuza, kufananisha thamani zao na pesa.
Kiukweli mwanadamu ana thamani kubwa sana. Tunaitambua thamani ya mwanadamu kwenye biblia ambapo Yesu aliacha enzi na kushuka duniani ili kumuokoa mwanadamu. Thamani ya mwanadamu ingekuwa ni dhahabu Mungu angetumia dhahabu, ingekuwa fedha pia angetumia fedha, lakini kwa sababu thamani ya mwanadamu ni kubwa zaidi ya vyote hivyo, Mungu alimtoa Yesu.
Unataka kujua thamani ya mwili wako?Basi tazama madaktari wanapohangaika pindi mtu anapoharibu kiungo kimojawapo. Kuna miguu ya bandia kwa mfano, hii inapatikana kwa pesa nyingi sana, lakini bado ubora wake haufanani kabisa na miguu halisi. Maskini hawezi kumudu kutumia au kupewa mguu wa bandia, lakini hata hivyo Mungu amempa maskini mguu bure kabisa na ni mguu bora kuliko mguu wa bandia ambao ni ghali sana.
Watu hawaijui kweli kwa sababu hawasomi neno, hawana mahusiano na Mungu na wengine wanapuuzia yale wanayofundishwa (na mtu anayepuuzia mafundisho naye namuita hajui, hajui uzito wa kosa analolifanya, hajui maana ya hilo alifanyalo). Na baada ya hapo wanaangukia katika matatizo kama neno linavyosema;
Warumi 1:18 – 32
Kwa maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu waipingao kweli kwa uovu.
Kwa kuwa mambo ya Mungu yanayojulikana yamekuwa dhahiri ndani yao, kwa maana Mungu aliwadhihirishia.
Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru;
kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza.
Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika;
wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo.
Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao.
Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.
Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;
wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.
Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.
Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya,
wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao,
wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema;
ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.
Hata kama umesoma vipi na unadhani unafahamu neno la Mungu vipi, bado usipofuata amri za Mungu wewe hauna ufahamu na hauijui kweli ya Mungu. Akili yako imefumbwa kwa sababu hujamruhusu Roho wa Mungu akufunulie kweli halisi ya ubaya wa hilo unalolifanya. Umepumbazika baada ya kumuweka Mungu pembeni na kutokukubali maonyo yake na neno lake likuongoze katika maisha yako. Maisha yako yamechafuka kwa sababu umeikataa kweli, na hauijui kweli ya Mungu iwezayo kukuokoa.
Hakuna sababu yoyote inayoweza ku – justify dhambi; ila watu wamejilegeza na kuipenda dhambi wakaiangukia bila kumgeukia Mungu awatetee.
Zifuatazo ni sababu nyingine, ambazo kwa kiasi kikubwa mzizi wake mkuu ni kutoifahamu kweli ya Mungu au kuipuuzia na kukataa uongozi wa Mungu katika maisha.
Tamaa za mwili
Yakobo 1:14-15Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.
Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.
Watu huzini kwa sababu ya kutawaliwa na tamaa za mwili, mwili unataka kuzini kwani ndiyo starehe na kitu cha kufurahisha kwake. Hapa katika tamaa za mwili, tamaa hizi husababishwa na vitu kadhaa, kwanza wengine huwa na roho za kurithi, ambapo kimaagano watu hawa huwa wanakaliwa na roho za uzinzi.
Suala hili lipo katika familia nyingi ambapo unakuta familia husika inafahamika, au ukoo husika unafahamika kuwa watu wake hutumikishwa sana na umalaya na uzinzi.
Pili tamaa za mwili huwa zinaendekezwa na kupewa nafasi na watu, hata wale ambao hawasumbuliwi na roho za uzinzi za kiukoo, bali wameziendekeza zile tamaa zinazowajia kama tu wanadamu wa kawaida. Wengine huingiwa na tamaa hizo mara baada ya kuanza kujihusisha na ngono kwa hiari au kwa kulazimishwa. Rafiki yangu mmoja alikuwa akimnukuu dada mmoja akisema dada huyo alikuwa anasema kwamba anamruhusu pasta/mchungaji amtoe mapepo yote ila asitoe pepo la uzinzi. Unaona kuwa huyu sasa anawaka tamaa muda wote na hataki hata kusikia tena mambo ya Mungu na hahitaji uponyaji katika tabia yake hii.
Vishawishi na kushindwa kujizuia
Kuna vishawishi ambavyo hutokea ambavyo ni vya hatari, kwa mfano kijana mmoja anaweza kulazimishwa au akatakiwa kufanya mapenzi na mke wa bosi wake kama ambavyo ilitokea kwa Yusufu. Majimama wanawapata vijana wengi sana wa aina ya Yusufu kwa sababu ya nguvu yao kubwa ya ushawishi.
Pia wapo watu wazima/wababa ambao wanatumia nguvu zao za ushawishi kuwashawishi wasichana wadogo na kuwaingiza katika tabia za uzinifu. Hili linatokea kwa wanafunzi, wanaoshawishiwa na walimu wao, au wanashawishiwa na watu wazima wengine, wa karibu au mbali. Mtoto mdogo, au binti, bado hajaelewa hasa ni kitu gani anachokifanya na akili yake haijakomaa vya kutosha kuweza kuchanganua mambo; watu wazima hawa kwa kulifahamu hilo, wanatumia nafasi hiyo kuwatumikisha watoto hawa katika ngono.
Jambo hili pia lipo majumbani, kwa wasichana wa kazi au wasichana wanaoishi na mama zao wadogo au ndugu zao wengine. Hili jambo linatokea sana na inashauriwa wadada wenye ndoa zao wawachunge wasichana wanaoishi nao ili wasitoe nafasi kwa wasichana hawa kupata vishawishi vya aina hii. Lakini hili pia linatakiwa liambatane na maombi ya mara kwa mara ili hofu ya Mungu na ulinzi wa Mungu uchukue nafasi zaidi. Usimwamini mumeo kupita kiasi kwani naye ni mwanadamu.
Vishawishi vingine vinatokea katika mazingira ambayo wahusika wanakuwepo. Hii inatokea pale ambapo mwanaume na mwanamke wanakuwa katika mazingira hatarishi yanayosababisha washawishike kuzini. Katika mazingira fulani watu wawili wanaweza kujikuta wakiwa faragha, na kama ilivyo ada ya miili, hujikuta wamevutwa na kushawishika kuongelea zinaa na hata kuzini. Mazingira haya yanaweza kuwa hayakupangwa na wote wawili, au yamepangwa na mmoja wao. Kwa kawaida mwanamke na mwanaume wakikaa peke yao wakaongea mambo mawili matatu, jambo la nne uwezekano ni mkubwa sana wakatumbukia kwenye mapenzi, kwani akili zao zinaanza kudadisi uhalisia wa maumbile. Hali inakuwa mbaya hata kama hawana mahusiano, na inakuwa ya hatari kupitiliza wakiwa kwenye mahusiano, hata kama wameokoka.
Kuna wakati inaweza kutokea mwanamke na mwanaume wakajikuta wanalazimika kulala pamoja, kwa sababu yoyote ile isiyozuilika. Epuka mazingira ambayo yanaweza kukufanya ukashawishika kuzini, Hata kama una nguvu kiasi gani ya Mungu, epuka mazingira kama haya kwani nguvu utakayotumia kuepuka mazingira haya ni ndogo kuliko nguvu inayotakiwa kujizuia kuzini pale unapojikuta umelala na mtu wa jinsia tofauti.
Unaweza kusema kwamba labda mtu anayelazimishwa na mazingira kuzini ni mzinifu toka mwanzo. La hasha, kuna watu kweli ni wazinifu ila mazingira yanawakumbusha na kuwafanya wazini bila kukusudia. Ni kama mwizi, kuna mtu anakuwa hana mpango wa kuiba, ila akipita kwako akakuta mlango uko wazi na ndani kuna vitu vya thamani, ataiba.
Pia kuna suala la dhambi kukaa ndani ya mtu. Kuna walokole duniani hapa hawafanyi dhambi siyo kwa sababu wametakaswa, la, ila ni kwa sababu hawajapata access ya dhambi hizo. Sasa watu wengi sana wana tabia ya kuwaamini watumishi wa Mungu kupita kiasi, eti unakuta mtumishi wa Mungu amefikia gesti halafu binti unaenda kuombewa huko na unaenda peke yako. Acha huo mchezo, wewe hata ukibakwa hakuna atakayekuelewa.
Biblia inatutuma kuwa wapole kama hua na kuwa na busara kama nyoka. Fanya maamuzi sahihi dada yangu, ukifika machinjioni ni kuchinjwa tu. Na hata wewe kaka pia, angalia sana unapofanya miadi na wadada, usijefanana na kondoo apelekwaye machinjioni.
Mithali 7:4-24
Mwambie hekima, Wewe ndiwe umbu langu; Mwite ufahamu jamaa yako mwanamke.
Wapate kukulinda na malaya, Na mgeni akubembelezaye kwa maneno yake.
Maana katika dirisha la nyumba yangu Nalichungulia katika shubaka yake;
Nikaona katikati ya wajinga, Nikamtambua miongoni mwa vijana, Kijana mmoja asiyekuwa na akili,
Akipita njiani karibu na pembe yake, Akiishika njia iendayo nyumbani kwake,
Wakati wa magharibi, wakati wa jioni, Usiku wa manane, gizani.
Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo;
Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake.
Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia.
Basi akamshika, akambusu, Akamwambia kwa uso usio na haya,
Kwangu ziko sadaka za amani; Leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu;
Ndiyo maana nikatoka nikulaki, Nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona.
Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari.
Nimetia kitanda changu manukato, Manemane na udi na mdalasini.
Haya, na tushibe upendo hata asubuhi, Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba.
Maana mume wangu hayumo nyumbani, Amekwenda safari ya mbali;
Amechukua mfuko wa fedha mkononi; Atarudi wakati wa mwezi mpevu.
Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.
Huyo akafuatana naye mara hiyo, Kama vile ng'ombe aendavyo machinjoni; Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu;
Hata mshale umchome maini; Kama ndege aendaye haraka mtegoni; Wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake.
Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Mkayaangalie maneno ya kinywa changu.
Usikose kufuatilia sehemu ya tatu ya somo hili. Mungu akubariki sana
No comments:
Post a Comment