Monday, September 26, 2016

HAKIKISHA UNATEMBEA KWENYE NJIA SAHIHI



“Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.” (Isaya 35:8)
Bwana Yesu Kristo asfiwe!

Neno la Mungu linatufundisha kuwa katika safari ya mtu hapa duniani pana njia kuu mbili anazoweza kupita. Njia moja inampeleka uzimani (mbinguni) na nyingine ni ile inayompeleka mautini (jehanamu). Yesu Kristo alitupa sifa za kila njia na akatuelekeza njia ya kuifuata, anasema:
Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache. (Mathayo 7:13-14)
Sifa ya njia ya upotevuni ni kuwa hiyo njia ni pana na ina watu wengi wanaoenda katika njia hiyo. Hii ni njia inayohusisha maovu yote ya ulimwengu. Dhambi, dhuluma, ufisadi, uasherati, uzinzi, uongo na matendo yafananayo na hayo yote ni mambo yanafanyika katika njia hii iendayo upotevuni (jehanamu). Yesu anasema njia hii ina watu wengi sana wanaoipita. Ni kweli kabisa hata ukiangalia kwa macho ya kawaida tu utagundua kuwa watu wengi sana wanavutwa kila siku katika anasa za dunia na kumsahau Mungu wao. Watu wengi wamewekeza muda wao na nguvu zao katika kujifurahisha katika raha za ulimwengu huu na hawataki kusikia habari za tumaini lililo katika Kristo Yesu, Bwana wetu.

Lakini taarifa mbaya kuhusu njia hii ni kuwa mwisho wake ni upotevu (mauti). Musa, mtumishi wa Mungu, alikataa kuiendea njia ya Misri japokua alikua amelelewa katika njia hiyo na kufundishwa hekima yote ya kimisri. Waebrania 11: 24-26 inatufundisha kuwa alifanya hivo kwa kuwa alijua hiyo raha ni ya kitambo tu, hivyo akaamua kuambatana na njia itakayompeleka kwenye raha ya milele.
Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo.

Watu wengi wanaindea njia ya upotevuni kwa sababu njia hiyo ndiyo yenye raha na anasa zote za hapa duniani. Lakini watu hawa akili zao zimefungwa wasijue yakuwa raha hizo ni za kitambo tu. Musa alikataa kujifurahisha katika raha za kitambo maana hazina thamani. Akakubali kuteseka pamoja na watu wa Mungu ili apokee raha ile ya milele iliyo katika Kristo Yesu.

Ndio! Njia ya pili ina sifa hiyo. Ni njia yenye mateso. Ni njia nyenye dhiki nyingi. Ni njia isiyopendwa na wengi kwa sababu haina umaarufu wala anasa zozote ndani yake. Lakini licha ya hayo yote njia hiyo ndiyo iendayo uzimani. Yesu anasema wanaopita katika njia hiyo ni wachache sana kwa sababu njia yenyewe imesonga na mlango wake ni mwembamba sana. Watu wanaosafiri katika njia hii mara nyingi wametafsiriwa kama wajinga au waliokosa kazi za kufanya. Na kwa sababu watu wengi hatupendi kupata shida, tumeikataa njia hii tukaichagua njia ile pana.

Lakini Isaya anazungumza kwa namna ya ajabu sana juu ya njia hii iendayo uzimani; anasema:
Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo. (Isaya 35:8)

Isaya anasema hiyo njia ina sifa kuu nne:

MOJA, njia hiyo ina JINA lake maalumu (inaitwa, Njia ya utakatifu). Maana yake mtu anaweza akaielewa njia hiyo na akaifuata. Na vile vile mtu asiyetaka kuindea njia hiyo anaweza tu kusoma kibao cha jina la njia hiyo akageuka akaenda zake. Ndio! Barabara nyingi za mijini zina majina yake, mfano, barabara ya Ali Hassan Mwinyi, barabara ya Mandela n.k. Lengo la kuzipa majina barabara (njia) hizi ni ili kumsaidia mtembeaji ajue kama yuko kwenye njia inayompeleka anakotaka kwenda. Pia ni kumsaidia mtu mwingine kumwelekeza mtembeaji mahali pa kupita ili kufika anakotaka kwenda.
Nivyo ilivyo kwa njia hii iendayo uzimani. Imepewa jina maalumu ili kuwasaidia wasafiri kuchagua kama wanataka kuipita au wabadilishe mwelekeo. Yesu Kristo anajitangaza kuwa yeye ndiye hiyo njia, anasema:
Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. (Yohana 14:6)

Yesu anajitangaza wazi wazi kuwa yeye ndiye njia ya kwenda kwa Baba. Maana yake anatujulisha kuwa wale wanaopita kwenye njia hii ni wale tu wanaoenda kwa Baba, kama mtu hana nia ya kwenda kwa Baba basi apite njia nyingine tu.
Sasa unahitaji kuelewa kuwa Yesu hazungumzii kwenda kwa Baba kwa maana ya maisha baada ya kufa tu. Anazungumzia utaratibu wa kumfikia Mungu Baba kwa haja yoyote ile kuwa lazima uanzie kwake. Maana yake kuna njia moja tu inayoweza kukufikisha kwa Baba, nayo ni Yesu – No shortcut, No alternative.

PILI, njia hiyo ina VIGEZO vya mtu kuipita. Isaya anasema “wasio safi hawatapita juu yake”. Maana yake ni kuwa kigezo cha mtu kupita juu ya njia hiyo ni lazima awe safi (awe ametakaswa). Ooh kumbe ndo maana Yesu alisema ‘Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni’ (Mathayo 7:20). Kigezo cha kupita juu ya njia hiyo sio kutaja jina la njia ila ni utakatifu. Mtu akiyafanya mapenzi ya Mungu mtu huyu anakua ametakaswa na hivyo anakua nayo sifa ya kupita juu ya njia hiyo.

Anhaa! Kumbe unaweza ukaiendea njia lakini ukashindwa kuipita kwa sababu umekosa sifa za kupita juu ya njia hiyo. Ngoja nitumie mfano wa daraja la kigamboni! Kila gari inayopita kwenye daraja lile inapaswa kulipa gharama za kupita pale darajani ndipo iruhusiwe kupita juu yake. Kwa hiyo kufika darajani na gari yako haimaanishi unaruhusa ya kupita. Ruhusa inakuja mara baada ya kuwa umelipa gharama. Hivyo ndivyo ilivyo pia katika kupita katika njia hii iendayo uzimani. Gharama yake ni UTAKATIFU. Watu wengi hatuko tayari kulipa gharama hiyo na hivyo tumeamua kuachana na njia hiyo. Lakini hata huko tulikoamua kupita kuna gharama yake, tena kubwa kuliko hii ya UTAKATIFU.

TATU, njia hii ni kwa ajiri ya wale WASAFIRIO. Hii ni neno linamaanisha kusudi au nia. Hakuna mtu anayeamka asubuhi na mapema akasenda stendi ya mabasi na mizigo yake wakati hana nia ya kusafiri. Tukimuuliza mwenzetu vipi? Anajabu: ‘aaa nimekuja tu hapa stendi kisha narudi nyumbani’. Tukimuona mtu wa namna hiyo lazima tushangae. Hatushangai yeye kwenda stendi na mizigo ila tunashangaa kwenda stendi na mizigo wakati hasafiri.

Isaya anasema njia hii ya UTAKATIFU ni kwa ajili tu ya hao wasafirio. Hao ndio walio na utayari na nia ya kulipa gharama ya kusafiri kupitia njia hiyo. Kama mtu hana nia ya kusafiri hawezi kupita njia hiyo maana ataona ni usumbufu. Lakini swali ni je, ni mtu yupi hapa duniani ambaye si msafiri? Ni yupi huyo ambaye hapa duniani ndio makazi yake ya milele? Kama hakuna, basi wote tu wasafiri. Na kama wote tu wasafiri basi tunapaswa kulipa gharama ya usafiri. Gharama yenyewe ni UTAKATIFU, na wengi hatuko tayari kulipa hiyo gharama.

Lakini msafiri ambaye hayuko tayari kulipa gharama za usafiri ni wazi kuwa hatafika anakotaka kwenda. Na ndivyo watu wengi ambavyo wataishia kwenda katika njia ya upotevuni kwa sababu moja tu – hawako tayari kulipa gharama ya kusafiri katika njia iendayo uzimani.

NNE, ishara ya kujua kama uko kwenye njia hiyo ni KUTOPOTEA. Isaya anasema wale waendao katika njia hiyo hata wajapokuwa wajinga HAWATAPOTEA. Hili ni neno la kutia nguvu sana kwa wale wasafirio katika njia hiyo. Wamehakikishiwa kufika salama. Hakuna kitu kizuri kwa abiri kuwa na uhakika na safari yake kuwa atafika salama hata kama atasinzia njiani.

Kwa nini hawatapotea? Ni kwa sababu mwenye njia mwenyewe amesema: Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama’ (Zaburi 32:8). Mwenye njia amewahakikishia wasafiri wake kuwa atawaonyesha njia; atawafundisha namna ya kutembea kwenye njia hiyo; wakishindwa atawashauri ni cha kufanya ili waendelee na safari; na hayo yote yatafanyika huku akiwatazama muda wote ili wasije WAKAPOTEA.

Ndio maana Yesu aliwahakikishia wanafunzi wake kuwa ‘mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari’ (Mathayo 28:20). Ni raha iliyoje kutembea katika njia hii ambayo umehakikishiwa usalama wako na kulindwa hadi ufike unakokwenda. Isaya anasema kuwa wale wanaoenda kwenye njia hiyo wanaweza wakaitwa wajinga, lakini hata kwa ujinga huo bado HAWATAPOTEA. Ndiyo maana mtume Paulo alipa ujasiri wa kumwambia mfame Feliki kuwa ‘…kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii (Matendo 24:14). Anasema hata kama ninyi mnasema njia hii ni uzushi, bado mimi naamini katika njia hiyo na ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu.

JIPIME KAMA HUJAPOTEA NJIA

Kigezo cha kujua kama uko kwenye njia iendayo uzimani ni KUTOPOTEA. Hebu angalia vizuri njia ulioko na ujiulize je, sijapotea? Chunguza matendo yake, chunguza matunda ya imani yako, chunguza marafiki ulionao, pima utayari wako wa kulipa gharama ya utakatifu, angalia utayari wako wa kujitoa kwa ajili ya Bwana kisha jiulize mara mbili mbili JE, SIJAPOTEA. Kumbuka kigezo cha njia hii ni kutopotea, na ndio maana ile njia nyingine inaitwa NJIA YA UPOTEVUNI kwa sababu wanaenda juu ya njia hiyo ni wale waliopotea.
Usijipime kwa kwenda kwako kanisani ukasema, sijapotea. Usiangalie kiwango chako cha kuomba ukasema, sijapotea. Usilinganishe utoaji wako wa sadaka ukasema, sijapotea. Hivyo vyote haviko kwenye sifa ya wale wasafirio katika njia hiyo. Sifa ya wale wasafirio katika njia hiyo ni UTAKATIFU, ndio maana njia yenyewe inaitwa Njia ya utakatifu. Lazima tuwe watakatifu ndipo tuwe na uhalali wa kumwendea Mungu Baba kupitia njia hiyo.

Watu wengi wanafikiri kuwa sadaka ni kigezo cha Mungu kusikia maombi yao. Wala hata! Mungu hana shida na sadaka yako – anahitaji moyo wako uwe safi. Ndiyo maana “heri wenye moyo safi, maana hao watamwona Mungu’ (Mathayo 5:8). Sipingi nafasi ya sadaka katika kukusogeza karibu na Mungu. Ila nasema sadaka sio priority (sio kipaumbele) cha Mungu. Angalia mtunga Zaburi anachosema:
Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau (Zaburi 51:16-17).

Kisha sikia nabii Mika 6:6-8 anavyosema:
Nimkaribie Bwana na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka za kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja? Je! Bwana atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu? Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!

Mungu anatafuta watu wenye roho iliyopendeka, wenye kutenda haki na kwenda kwa unyenyekevu mbele za Mungu wao na kufanya mapenzi ya Mungu. Hao ndio waiendeao njia hiyo iendayo uzimani. Nataka nikutie moyo kuwa tunaye Bwana wa vyote. Ameahidi kuhakikisha kuwa hatupotei kwenye njia hiyo. Kazi yetu ni kukubali atutuongoze tu basi. Kumbuka wakati Israeli wanatoka Misri waliongozwa kwa wingu mchana na nguzo ya moto usiku ili wasije wakapotea njia mpaka walipoingia kanaani. Jipime mpendwa wangu, wewe uko kwenye njia gani? Kama ni njia ya upotevuni – kama umepotea, basi rudi. Yesu anakuita, anataka atembee na wewe ili akufikishe kwa Baba. Kama hujapotea, basi nakutia moyo mpendwa wangu – piga moyo konde hata kama wengine wanakuona mjinga, songa mbele. HAUTAPOTEA KAMWE.
Mwl. LUKIKO, L

No comments:

Post a Comment