Mwandishi: Anderson Leng'oko
Utangulizi
Mpendwa msomaji; tulijifunza toka katika sehemu ya kwanza kuwa zipo faida nyingi za kuwa na mahusiano binafsi na Mungu. Tunaendelea
na faida hizo. Lengo la kuzijadili faida hizi ni kuwafanya watu wawe na uwezo
wa kuwasiliana na Mungu muda wote na wamjue Mungu binafsi. Lengo kuu ni kuwafanya
watu kuwa na uhusiano binafsi na Mungu na wamweke Mungu mbele na karibu nao
kuliko mtu mwingine yeyote. Baada ya kulisoma somo hili Mungu akusaidie kukuza
mahusiano yako binafsi na Mungu ili uweze kumgeukia yeye katika kila changamoto
unayokutana nayo.
Faida
za kuwa na mahusiano binafsi na Mungu (zinaendelea)
Kuepuka
kukatishwa tamaa
Watu unaowatafuta wakuombee na kuwashirikisha shida
zako wanaweza kukukatisha tamaa kutokana na kuwa hawana mzigo na hawayaoni
maumivu halisi unayopata kulingana na uzito ulionao katika shida husika. Kwa
hivyo namna watakayokuhudumia inaweza isiwe ya kutosha kuliondoa tatizo lako.
Yesu alikuwa anaomba na wanafunzi wake, lakini kutokana na jinsi walivyokuwa
hawajui ni namna gani wangeweza kumsaidia au kumtia nguvu, walijikuta wanalala
katika wakati ambao Yesu alikuwa anahitaji sana msaada wao. Kwa hivyo Yesu,
kama asingekuwa na mahusiano binafsi na Mungu akawa anawategemea wanafunzi wake
kama kiunganisho kati ya yeye na Mungu, basi ingekuwa shida sana kwake.
Mathayo 26:37-45
Akamchukua Petro na
wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka.
Ndipo akawaambia,
Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.
Akaendelea mbele
kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana,
kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo
wewe.
Akawajia wale
wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja
nami hata saa moja?
Kesheni, mwombe,
msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.
Akaenda tena mara ya
pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke
nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe.
Akaja tena, akawakuta
wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito.
Akawaacha tena,
akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale.
Kisha akawajia
wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na
Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi.
Kipo kisa kimoja mimi kilinitokea miaka kadhaa
iliyopita. Baada ya mama yangu mzazi kuugua Kansa kwa muda mrefu alifariki.
Alipokuwa amefariki mimi nilienda kwenye mazishi yake pamoja na wenzangu, wa
Fimbo ya Musa. Tulipofika mazishini dada yake mama yaani mama mkubwa tulimkuta
akiwa anaumwa sana, ugonjwa wa kutisha ambao ulikuwa umepelekea hadi akili zake
kuyumba. Alikuwa hawezi kusimama kwenye jua hata kwa dakika tano.
Sasa kwa kuwa mimi nilikuwa nimesema na Mungu kwa
muda mrefu sana kuhusu ugonjwa wake huu, nilifurahia sana hatua ya Fimbo ya
Musa ministry kuwepo pale kwani ilikuwa ni fursa nzuri sana ya kumuombea mama
huyu.
Sasa baada ya kuwa tumeamua kumuombea mama mkubwa
wangu tulienda kanisani ambako tulikuta viongozi wa kanisa ambao waliamua
kutusaidia kuomba. Tulipokuwa tumeomba kwa muda mfupi kiongozi wa kanisa
alianza kukatisha maombi ili afunge kipindi tuondoke. Hii ilitokea kwa sababu
alikuwa hajui hasa mimi nilikuwa na mzigo kiasi gani juu ya huyu mama.
Nilikuwa nimemlilia Mungu kwa takribani mwaka mzima
sasa kuhusu mama huyu kwani tatizo lake hilo lilikuwa limemsumbua kwa muda
mrefu. Sasa hapa nilikuwa nimewasihi wana Fimbo ya Musa wanisaidie kuomba usiku
huu kwani wao walitaka waondoke mara tu baada ya mazishi. Lakini nilipowaomba
wabaki tumuombee mama mkubwa walikubali hivyo tukaamua tukafanye maombi. Sasa
haiwezekani maombezi yaliyosababisha watu wakatishe safari yakaombwa kwa dakika
kumi.
Sisemi kwamba maombi lazima yawe ya muda mrefu ili
yajibiwe, ninachotaka hapa kusema ni kwamba siku ile mzigo niliokuwa nao mimi
juu ya maombezi yale ulikuwa ni mkubwa sana hadi nilikuwa niko tayari hata
kukesha kama mama mkubwa asingefunguliwa. Ni siku ambayo sitaisahau katika
maisha yangu kwani Mungu alinipa nguvu ya ajabu sana kiasi kwamba nikaweza
kwenda kufanya huduma nikiwa nimetoka kumzika mama yangu mzazi saa moja au
mawili yaliyopita.
Hili lilikuwa ni jambo kubwa sana kwangu, kwani
miezi mitatu iliyopita kabla ya hapo nilikuwa nimeoneshwa maono nikimuombea mama
Mkubwa na siku hiyo tulipokuwa tunamuombea ilitokea ikawa vilevile kama
nilivyoona kwenye maono na ilikuwa ni utimilivu wa yale maono kunihakikishia
kwamba yale mambo tulikuwa hatuyafanyi kwa utashi wetu. Hivyo isingekuwa rahisi
kwetu kuacha maombi eti tu kwa sababu kiongozi wa kanisa ameamua kuahirisha
maombi ili awahi kwenye mkesha kule msibani (ambako ni kwetu).
Tulimwambia yule kiongozi wa kanisa kwamba kama walikuwa
na haraka waende, na kweli tuliwaruhusu tukaendelea na maombi hadi mama mkubwa
alipofunguliwa. Hii ndiyo faida ya kuwa na mahusiano binafsi na
Mungu. Hautegemei mtu mwingine katika kuyashughulikia mambo yako. Unapokea amri
kutoka juu na ni Mungu peke yake anayeweza kukwambia jambo ukalifuata na yeye
uwe na hakika kwamba hatakuacha kamwe kwani ni rafiki yako wa karibu kuliko mtu
mwingine yeyote hapa duniani.
Kwa hiyo kwenye mfano wa hapo juu tumeona kuwa
tulikuwa na mzigo wetu binafsi na tulikuwa na nguvu za Mungu za kwetu ndani
yetu, hatukuwa tunategemea viongozi wa kanisa, na kusema kweli hata tulipokuwa
tunaanza kuomba pamoja nao tulitamani watupishe toka mwanzo; Haleluya!
Uwezo wa kukutana na
Mungu moja kwa moja kama wewe, wala siyo kwa kupitia kwa mtu mwingine
Katika biblia kuna mifano ya watu kadha wa kadha waliotumia watu
kumtafuta Mungu. Wana wa Israeli walimtumia Samweli kumtafuta au kukutana na
Mungu, matokeo yake Samweli alipokaribia kufa walijawa na hofu kubwa na
wakajikuta wanaomba mfalme; jambo ambalo Mungu hakulipenda hata kidogo.
1
Samuel 8:1-22
Hata Samweli
alipokuwa mzee, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli.
Na jina la mwanawe
mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi
katika Beer-sheba.
Ila wanawe hawakuenda
katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na
kupotosha hukumu.
Ndipo wazee wote wa
Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama;
wakamwambia, Angalia,
wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme
atuamue, mfano wa mataifa yote.
Lakini neno hilo
likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli
akamwomba Bwana.
Bwana akamwambia
Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa
maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.
Kwa kadiri ya matendo
yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa
kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe.
Basi sasa, isikilize
sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya mfalme
atakayewamiliki.
Naye Samweli
akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya Bwana.
Akasema, Mfalme
atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka
kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya
magari yake.
Naye atawaweka kwake
kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka
walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na
vyombo vya magari yake.
Na binti zenu
atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji.
Atatwaa makonde yenu,
na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili
awape watumishi wake.
Naye atawatoza ushuru
wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake.
Atawatwaa watumishi
wenu na wajakazi wenu, na ng'ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye
atawatia katika kazi zake mwenyewe.
Atawatoza fungu la
kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake.
Nanyi mtalia siku ile
kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; Bwana asiwajibu siku ile.
Walakini hao watu
wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka
kuwa na mfalme juu yetu;
ili sisi nasi
tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atoke mbele yetu
na kutupigia vita vyetu.
Samweli akayasikia
maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa Bwana.
Bwana akamwambia
Samweli, Isikilize sauti yao, ukawafanyie mfalme. Kisha Samweli akawaambia watu
wa Israeli, Enendeni kila mtu mjini kwake.
Samweli aliwatawala wana wa Israeli na alikuwa ni nabii juu yao.
Lakini kutokana na kuwa wana wa Israeli walimtumia Samweli kukutana na Mungu,
walijawa na hofu walipoona Samweli anakaribia kufa kwani walijua kwamba
hawangekuwa na mtu ambaye angekuwa anawasiliana moja kwa moja na Mungu Samweli
akishakufa. Huu ni udhaifu waliokuwa nao hawa wana wa Israeli, wangekuwa
wamemjua Mungu ipasavyo na wana mahusiano binafsi na Mungu kila mmoja wao, basi
wangekuwa na Roho wa Mungu ambaye angekuwa amewafunulia makusudi ya Mungu juu
ya jambo hili na wangefuata mashauri ya Mungu badala ya kung’ang’ania mfalme.
Unapokuwa una mtu unayemtegemea akupeleke mbele za Mungu utayumba
sana kiroho kwani huyu mtu akifa au akikuchoka hauna namna ya kuwasiliana na
Mungu moja kwa moja.
Mungu akiishi na wewe atakuwa na mambo anayotaka uyafanye wewe
kama wewe kwa kufuata mashauri yake. Wala hautafanya kwa kufuata wengine, kama
Waisraeli wanavyosema kwamba tupe mfalme kama ambavyo wenzetu wengine wana
mfalme.
Sikatai kwamba Mungu huwa anatumia watu kukutana na sisi muda
mwingine; ninachotaka ujue hapa ni kwamba unatakiwa kuwa na mahusiano na Mungu
ya moja kwa moja licha ya kuwa kuna watu ambao Mungu anaweza kuamua kuwatumia.
Usikose sehemu ijayo ili tupate nafasi ya kuliangalia suala hili
kwa kina zaidi… wakaribishe na wengine wajifunze kutoka kwa Roho wa Bwana
katika somo hili.
No comments:
Post a Comment