Mwandishi: Anderson Leng'oko
UTANGULIZI
Hili ni somo linalohusu maombi binafsi wakati
unaokumbwa na tatizo kubwa ambalo linaweza hata kugharimu maisha yako. Ni
wakati ambao unamuhitaji sana Mungu na hata huna muda wa kumtafuta mtu
akusaidie kuomba. Unajikuta umebaki moyoni mwako wewe na Mungu wako hivyo
unatakiwa kupeleka hoja na kumsihi Mungu akurehemu katika gumu upitialo.
MSITARI WA SOMO
Msitari wa somo hili unatoka
katika kitabu cha Isaya
38:1-6
Siku hizo Hezekia
aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda
kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana
utakufa, wala hutapona.
Basi Hezekia
akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana,
akasema, Ee Bwana,
kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo
mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.
Ikawa, neno la Bwana
likamjia Isaya, kusema,
Enenda ukamwambie
Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako,
nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na
mitano.
Nami nitakuokoa wewe,
na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.
HABARI ZA HEZEKIA
Hezekia alikuwa mfalme wa Israeli, yeye huyu mfalme anatajwa kuwa
alikuwa mwaminifu sana mbele za Bwana jambo ambalo lilimfanya apendwe na Mungu
na katika wakati wa utawala wake Mungu aliwapiga wapinzani wa Israeli kwa mkono
wake mwenyewe.
Hata hivyo ilifikia kipindi kama tulivyoona katika
maandiko tunayosimamia katika somo hili kwamba Hezekia aliugua. Ugonjwa huu
ulimfanya Mungu amtume nabii Isaya aende akamwambie Hezekia kwamba atengeneze
mambo ya nyumba yake kwa maana ni ugonjwa ambao Hezekia asingepona.
Katika hali ya kawaida, Hezekia angekuwa ni mtu wa
kawaida angeheshimu sauti ya nabii na kuandaa mambo ya nyumba yake. Lakini
badala yake tunaona Hezekia akijigeuza, na kuelekeza uso wake ukutani,
akimwomba Bwana.
Kwa kuwa Mungu ni mwaminifu na wa haki, anamsikia
Hezekia na kumpa haja za moyo wake kama tulivyoona hapo juu ambapo anamuongezea
miaka kumi na tano ya kuishi.
MAMBO YA KUJIFUNZA KUTOKA KWA HEZEKIA
HEZEKIA
ALIKUWA NA MAHUSIANO BINAFSI NA MUNGU
Watu wengi huwa wanadhani Mungu anahusiana na watu
kwa makundi. Mungu hahusiani na kanisa kama kundi bali Mungu anafanya mahusiano
binafsi na mtu.
Ezekiel
22:30
Nami nikatafuta mtu
miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali
palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.
Mungu kabla hajawa na mahusiano na kanisa zima, anatafuta kuwa na
mahusiano na mtu mmoja mmoja kwanza. Hawezi Mungu kukaa na kanisa kama hana
mahusiano na mtu mmojammoja kwenye hilo kanisa.
Ndiyo maana hata kwenye kuokoka wanasema unampokea Yesu Kristo
kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako; wala siyo kumpokea Yesu Kristo kama Bwana
na mwokozi wa kanisa lako. Tena wazungu wana msemo mzuri sana wanaposema “You
receive Jesus as your personal
saviour’’. Hili neno ‘personal savior’ lina maana ya mkombozi wako binafsi.
Kwa hiyo Yesu anakuwa mkombozi wako binafsi na siyo wa kanisa, yaani Yesu
anaanza kukuhudumia wewe kwanza halafu ndipo anahudumia kanisa kupitia wewe.
Faida za kuwa na mahusiano binafsi na Mungu
Mungu
anakuwa anashughulika na shida zako moja kwa moja
Mungu anataka shida zako azishughulikie yeye ili apate
sifa kupitia mafanikio yako. Mungu akishakuwa nyumbani kwako, moyoni mwako
anakuwa ndiyo mtu wa kwanza kujua shida zako kabla hata rafiki yako hajajua.
Hii inamfanya Mungu kushughulikia shida zako kwa wakati na kwa uhakika kabla
hazijakuumiza.
Mungu
anaweza kukutunzia siri zako
Mara nyingi sana watu wanakuwa na shida katika
maisha yao lakini shida hizo wasingependa kuzikuta mtaani zimemwagwa na kila
mtu anaziongelea. Mungu ndiye ajuaye sirini na yeye anaweza kukujibu na kukuhifadhi
hadi ukapata haja au jawabu la tatizo lako bila mtu mwingine kujua.
Mungu
ajuaye sirini ameahidi kuwajazi watu wamwombao
Mathayo
6:6
Bali wewe usalipo,
ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali
mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
Yametokea matatizo mengi sana katika kanisa pale
ambapo mpendwa unakuwa na tatizo lako na unaamua kuwashirikisha wapendwa
wakuombee lakini matokeo yake wanaenda kukutangaza kwa watu na kukucheka
mtaani. Hiyo isikusumbue, tengeneza mahusiano binafsi na Mungu ili uwe na uwezo
wa kupambanua mambo ya kuwaambia watu na ya kubaki nayo mwenyewe. Na pia
uhusiano mzuri na Mungu hukuepushia mambo ya fadhaa na matatizo kadha wa kadha
ambayo watu huyapata kwa kutokuwa na uhusiano binafsi na Mungu.
Msaada
wa karibu na wa haraka
Kuna wakati unahitaji msaada wa karibu na wa haraka
sana kwa ajili ya shida zako. Kuna wakati mtu anahitaji maombi ya haraka, au
wewe usiku wa manane umevamiwa na nguvu za giza, au mtoto wako mdogo sana
amevamiwa na nguvu za giza. Unachotakiwa kufanya hapa ni kugeukia ukutani na
kuomba kwa Mungu, na hii inakuwa ni rahisi sana kama utakuwa ni mtu wa
kuimarisha mahusiano yako binafsi na Mungu.
Kuna watu hulazimika kuwatafuta wachungaji usiku wa
manane kwa shida ambazo kimsingi kama wangetulia wenyewe na Mungu zingeweza
kutatuka tu. Lakini zinawasumbua na kuwapotezea muda mwingi sana kwa kuchelewa
kutafuta watu wa kuwaombea.
Watu kama hawa kwa kuchelewesha tatizo au kwa
kushindwa kupata watu wanaofaa hujikuta wakisumbuliwa hadi wanafikia kiwango
cha kugeukia miungu mingine iwatatulie shida zao wakidhani kuwa Mungu
ameshindwa au hawezi.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa kwa kukosa mahusiano
binafsi na Mungu wanakuwa hawana mizizi thabiti ya imani na hivyo kuyumbishwa
na matatizo.
Usikose kufuatilia sehemu ya pili ya somo hili, waalike na wengine pia washiriki nasi baraka hizi.
No comments:
Post a Comment