Tuesday, February 21, 2017

KUGEUKIA UKUTANI (SEHEMU YA SITA)

Mwandishi: Anderson Leng'oko

Utangulizi
Mpendwa msomaji, katika somo hili la kugeukia ukutani tumejifunza mambo kadha wa kadha na moja ya kipengele na hasa msitari wa somo tumeupata kwenye hadithi ya mfalme Hezekia. Katika sehemu hii tutaenda kujadili jambo kubwa sana tunaloweza kujifunza kutoka kwa Hezekia ili tukifanikiwa kuwa nalo hilo litusaidie kugeukia ukutani tunapokutana na changamoto maishani. Kwa kusoma sehemu nyingine za somo hili zilizotangulia bonyeza hapa.

HEZEKIA ALIKUWA NA MATENDO MEMA YA KUMPENDEZA MUNGU
Hezekia alikuwa na matendo mema aliyokuwa ameyafanya hapo kabla hajakutana na magumu haya ya kuugua.

Matendo haya mema yalimsaidia Hezekia kwenda mbele za Bwana kujenga hoja ya kwanini aongezewe miaka ya kuishi. Kwa Maneno mengine Hezekia alikuwa anamkumbusha Mungu jinsi ambavyo ameitumia miaka aliyopewa kwa uaminifu na hivyo kumfanya Mungu alazimike kumuongezea miaka.

Mungu anapenda kumuona mtu akiutumia vizuri muda aliompa ili aone faida ya mtu huyu kuishi miaka aliyoishi. Kwa ukweli Mungu anaweza kukupa mambo ya kufanya kulingana na umri atakaokupa, lakini kuna matendo ambayo ukiyafanya yatamfanya Mungu akuongezee miaka ya kuishi. Angalia ile amri ya tano inavyosema:


Kutoka 20:12
Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.

Lakini pia kuna mstari unasema

Mithali 10:27
Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.

Kwa hiyo tunaona kuwa mtu akiishi kwa matendo mema ataongezewa siku za kuishi. Ilikuwa rahisi kwa Mungu kumuongezea Hezekia miaka kutokana na ukweli kwamba ahadi ya Mungu ilikuwa ni kuongeza miaka kwa wale watendao mema ikiwemo kuwaheshimu baba na mama.
Hivyo tunahimizwa kutenda mema siyo kwa ajili ya wale tunaowatendea mema tu bali wafaidika wakubwa na wa kwanza wa matendo yetu mema ni sisi wenyewe kwani matendo yale yanaturudia na kutuongezea wingi wa siku na baraka tele katika maisha yetu. Haleluya!

Siku moja kaka yangu aliwahi kulalamika kuwa wanadamu siyo wema na hawafai kusaidiwa. Alisema kuwa leo unaweza kumsaidia mtu lakini kesho mtu huyo huyo anakutukana na kukudharau kana kwamba hukumsaidia. Nikamwambia palepale kwamba kumsaidia mtu ni jambo jema sana na kamwe usimsaidie mtu ukitarajia kupata mema kutoka kwake. Na kwa tahadhari ni bora ukajiandaa kisaikolojia kurejeshewa mabaya na mtu huyo ili ikishatokea usiumie sana.

Usitoe msaada kwa mentality kwamba/ kwa fikra kwamba utarejeshewa wema ulioutenda, bali tenda wema ili Mungu wako wa mbinguni akubariki na ujiongezee furaha na amani katika maisha yako;
Kuna methali ya kichina inasema kama unataka furaha itakayodumu maisha yako yote basi msaidie mtu.

Kusaidia watu huleta furaha katika maisha yote. Mimi kila nikikumbuka wale watu niliowasaidia na jinsi nilivyowasaidia huwa nafurahi sana na mara nyingi wale watu huwa siwakumbuki hata sura.
Niliwahi kumwambia rafiki yangu kuwa unapomsaidia mtu halafu akakurejeshea zile fadhili zako, umeshaipata thawabu yako, lakini ukimsaidia mtu halafu asikurejeshee fadhili, inalipa zaidi maana fadhili hizo zitarejeshwa na Mungu aliye mbinguni.

Sasa hebu tufanye mahesabu hapa kidogo… Kama ukimsaidia mtu halafu akakurejeshea thawabu inakuwa ni umeshalipwa tayari na usitarajie kukuta thawabu yako pengine, basi utatamani sana kufanya wema halafu usilipwe ili thawabu yako ipatikane kutoka kwa Mungu ambaye ni mwaminifu. Lakini tazama, kama ukimtendea mtu wema asirudishe, Mungu anakujazia na kukulipa mwenyewe; hii ina maana kuwa ukimtendea mtu wema halafu akakulipa mabaya, ile thawabu yako iliyo mbinguni inaongezeka maradufu; ili kufidia ule ubaya uliotendewa. Ila itaongezeka tu kama wewe hautamjibu vibaya wala kumsimanga kwa wema uliomtendea.

Mathayo 6:1
Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.

Luka 14:12-14
 Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo.  Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu,
 nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.

Kwa hiyo mpendwa, usitende wema ili uonekane na watu. Usiwe kama baadhi ya wanasiasa wanaojipanga kugombea ubunge  ambao hupiga picha wanapotoa misaada ili waje wawaambie watu baadaye kuwa wao ni wapenda watu. Kwa Mungu mambo yafanywayo kwa siri ndiyo yanalipa zaidi. Saidia bila kumwangalia mtu usoni, Mungu anakuona, atakulipa malipo ya haki. Ukitegemea kulipwa na uliyemsaidia shetani atatumia nafasi hiyo kukudhihaki na atamtumia mtu yuleyule uliyemsaidia kukuumiza!

Mwanadamu hawezi kukulipa ndugu usipoteze muda wako. Unamkosea Mungu unaposaidia mtu ukitegemea fadhila au malipo kutoka kwake, kanuni za kimungu haziko hivyo ndugu utaumia!

Sisi watumishi wa Mungu tunayaangalia yaliyo juu, wala hatuyaangalii yaliyo katika nchi.
Tunatoa kwa moyo wa ukarimu, hatutoi ili tupate sifa kwa watu. Tunatoa kwa sababu tumezaliwa kutoa na kubariki watu. Tena kuna wakati hata huko kutoa kusipoambatana na yale tunayoahidiwa sisi tunaendelea kutoa tu. Kwa sababu kutoa ndiyo asili yetu, furaha yetu ipo katika kusaidia watu bila kujali kama tunafaidika au la. Tukirudishiwa mema tunafurahi, tusiporudishiwa chochote tunafurahi vilevile na tukirudishiwa mabaya tunafurahi zaidi kwani twajua kuwa hilo la mwisho ndilo lenye thawabu kubwa kuliko zote! Haleluya!

Tumejifunza kuwa Hezekia hakusaidiwa na watu aliowasaidia katika shida yake; bali alisaidiwa na Mungu akiisha kumkumbusha jinsi alivyotenda mema. Hivyo ni vyema kutenda mema kwa ajili yetu wenyewe. Mungu akusaidie katika kutenda mema ili uwe na cha kukusaidia unapokumbwa na shida na kumgeukia Mungu kama Hezekia.


Usikose kuendelea kujifunza pamoja nasi. Mungu azidi kukubariki.

No comments:

Post a Comment