Thursday, November 10, 2016

MJI WA MAKIMBILIO

Mwandishi: Anderson Leng'oko 

Kuna miji katika Israeli ilikuwa imetengwa maalumu, nayo ikawa inaitwa miji ya makimbilio.Miji hii walikuwa wanakimbilia watu wanapokuwa wameua bila kukusudia. Ilikuwa kwamba ukiwa ulikuwa shambani kwa mfano, ukawa unafanya kazi na mwenzio halafu kwa bahati mbaya ukamuumiza au kumjeruhi hata akafa, unakuwa umeua na akitokea ndugu ya yule mtu anaweza akakuua kama sehemu ya kisasi na kamwe hatakuwa na hatia. 

Kwa kuliona hilo, kwamba kuna watu walikuwa wanaua bila kukusudia, Mungu aliwaamuru wana wa Israeli kutenga miji ya makimbilio. Ili watu kama hawa wakishaua wakimbilie huko, wasiuawe na walipa visasi. 

Ndipo ikawepo hiyo miji iitwayo miji ya nini jamani?Miji ya Makimbilio.

Sheria za miji ya makimbilio zilikuwa hivi:
Mtu ambaye ameua bila kukusudia tu ndiye aliyekuwa anakimbilia katika miji hii.Lakini pia mtu alikuwa anatakiwa kukaa katika miji hii hadi pale kuhani mkuu atakapokufa. Kwa wale ambao hatukai sana na biblia, Israeli kama taifa lilikuwa na watu maalumu kwa ajili ya kuwakutanisha na Mungu, watu hao walikuwa wanaitwa makuhani. Sasa makuhani walikuwa ni wengi na walikuwa na kuhani mkuu, ambaye ndiye alikuwa mkuu wa makuhani wote katika Israeli, kama wewe huwa unatembeatembea kwenye agano jipya utakuta kuna mahali wanasema wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu Kayafa.

Basi ukiua bila kukusudia ukakimbilia mji wa makimbilio, hautaguswa wala kulipizwa kisasi na utatakiwa kukaa humo humo ndani mpaka siku ambayo kuhani mkuu atakuwa amekufa, ndipo utaruhusiwa kutoka. Wakati kuhani mkuu hajafa, ukikutwa nje kidogo tu ya mji huo na mlipa kisasi, utauawa na aliyekuua atakuwa hana hatia. Mlipa kisasi hawezi kukuua kama utabaki ndani ya mji wa makimbilio. Ila kuhani mkuu aliye madarakani wakati unakimbilia katika mji huo atakapokuwa amekufa, basi utaruhusiwa kutoka katika mji huo wa makimbilio na kurudi katika mji wako wa nyumbani kwenu, ulikozaliwa, ambapo hakuna tena mtu atakayeruhusiwa kukuua, hata huyo mlipa kisasi mwenyewe.



Hesabu 35:10-28
Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani, Ndipo mtajiwekea miji iwe miji ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko. Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe. Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa kwenu ni miji sita ya makimbilio. Mtawapa miji mitatu ng'ambo ya pili ya Yordani, na miji mitatu mtawapa katika nchi ya Kanaani; miji hiyo itakuwa ni miji ya makimbilio. Miji hiyo sita itakuwa miji ya makimbilio kwa ajili ya wana wa Israeli, na kwa ajili ya mgeni, na kwa ajili ya huyo aketiye kati yao hali ya ugeni; ili kila amwuaye mtu, naye hakukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.

Lakini kama alimpiga kwa chombo cha chuma, akafa, ni mwuaji huyo; mwuaji hakika yake atauawa.Na kama alimpiga kwa jiwe lililokuwa mkononi mwake, ambalo kwa hilo humkini mtu kufa, naye akafa, yeye ni mwuaji; huyo mwuaji lazima atauawa. Au kama alimpiga kwa chombo cha mti kilichokuwa mkononi mwake ambacho kwa hicho humkini mtu kufa, naye akafa, ni mwuaji huyo, mwuaji lazima atauawa.Mwenye kutwaa kisasi cha damu ndiye atakayemwua mwuaji; hapo atakapokutana naye, atamwua.

Tena kwamba alimsukuma kwa kumchukia, au kwamba alimtupia kitu kwa kumvizia, hata akafa;au akampiga kwa mkono wake kwa kuwa ni adui, naye akafa; yeye aliyempiga lazima atauawa; yeye ni mwuaji; mwenye kutwaa kisasi cha damu atamwua mwuaji, hapo atakapokutana naye. 

Lakini ikiwa alimsukuma ghafula pasipo kumchukia; au akamtupia kitu cho chote pasipo kumvizia,au kwa jiwe liwalo lote, ambalo kwa kupigwa kwalo humkini mtu kufa, asipomwona, akamtupia hata akafa, naye hakuwa adui yake, wala hakumtakia madhara; ndipo mkutano utaamua kati ya huyo aliyempiga mtu na huyo atakayetwaa kisasi cha damu, kama hukumu hizi zilivyo; nao mkutano utamwokoa yule aliyemwua mtu na mkono wa mwenye kutwaa kisasi cha damu; tena mkutano utamrejeza katika mji wake wa makimbilio, aliokuwa anaukimbilia; naye atakaa humo hata kifo chake kuhani mkuu, aliyepakwa mafuta kwa mafuta matakatifu.

Lakini kama mwenye kumwua mtu akienda wakati wo wote kupita mpaka wa huo mji wa makimbilio, alioukimbilia;na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwona, naye yu nje ya mpaka wa mji wake wa makimbilio, na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwua huyo mwuaji, hatakuwa na hatia ya damu;kwa sababu ilimpasa kukaa ndani ya mji wake wa makimbilio hata kifo chake kuhani mkuu lakini kuhani mkuu atakapokwisha kufa huyo mwuaji atarudi aende nchi ya urithi wake.


Umeona sasa?
Tunachojifunza leo
Mji wa makimbilio katika maisha yetu ni Yesu Kristo, na yeye ndiye kuhani wetu mkuu.

Waebrania 6:20 alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.

Sisi wote tumetenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, hivyo tu wauaji kwa namna moja au nyingine, na tunastahili kufa, maana mshahara wa dhambi ni mauti, hivyo mlipa kisasi wetu shetani anatafuta atuue.

Warumi 3:23 kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;

Warumi 6:23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Warumi 8:13 kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.




Tukiwa kama watenda dhambi, tuna mshitaki wetu ambaye ni shetani, yeye anatushitaki kwa baba anatamani alipe kisasi. Lakini wokovu unaopatikana kwa kumpokea Yesu ndiyo mji wetu wa makimbilio, ambako tusipokimbilia, shetani atatuua. Lakini tukishakimbilia huko tena, tunatakiwa kukaa ndani ya mji, tukitoka kidogo tu, kwa mfano tukatenda dhambi na kuacha utakatifu, shetani atatuua.

Kuhani wetu mkuu ni Yesu, ambaye anaishi milele, hivyo kwa sababu yeye hafi, hatuwezi kurudi mijini kwetu tulikozaliwa, ambako ni dhambini, kwani tukitoka tu, kwa sababu kuhani wetu bado hajafa, mtwaa kisasi atatuua, hadi kuhani afe ndipo tunaweza kutoka, sasa huyu Yesu yeye ni kuhani milele mfano wa Melkizedeki, hivyo maadamu yeye yuko hai milele, sisi tutakaa katika mji wa makimbilio(yaani ndani yake) milele hata ije ile hukumu ya mwisho itakayotuweka huru na mtesi wetu ibilisi.

Ndugu yangu uliye dhambini, kimbilia kwenye mji wa makimbilio, mpokee Bwana Yesu na uishi ndani yake na usitoke kamwe.
Na wewe uliyekwishakumpokea Yesu usiondoke humo ndani, asije adui akakupata nje ya mji wa makimbilio akakuua. Ukapotea.

Yesuni mji wa makimbilio ulio bora zaidi kuliko ile miji ya makimbilio iliyokuwa Israeli, kwani ile miji watu waliokuwa wanaikimbilia na wameua kwa makusudi walikuwa wanakamatwa na kuuawa. Lakini Yesu anakukaribisha yeyote, hata wewe uliyetenda dhambi kwa kukusudia, hata kama hayo mauaji. Unasamehewa bure na unapewa zawadi ya uzima wa milele duniani na mbinguni haleluya!
Lakini pia Israeli ilikuwa na miji sita tu ya makimbilio, kwa maana kwamba ilikuwa michache na ukiwa huna mbio, mlipa kisasi akakukimbiza akakukamata kabla hujafika, basi unakufa. Lakini Yesu ni mji wa makimbilio aliye kila mahali! Yupo moyoni mwako anabisha, fungua aingie.
Yesu ndiye njia kweli na uzima, yeye ndiye huo ufufuo, Bwana wa mabwana, mpokee leo, ndiye mji wa makimbilio na ndani yake tunakaa salama mbali na mikono ya adui.
Yohana 14:6Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.

John 11:25 Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;

Yohana 6:37 Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe.

Kama wewe unayesoma somo hili unahitaji kumpokea Bwana Yesu Kristo, basi sema maneno haya kwa kumaanisha

Bwana Yesu, nakuja kwako, mimi ni mwenye dhambi, ninatubu, naomba unisamehe eeh Bwana, futa jina langu, kwenye kitabu cha hukumu, andika jina langu kwenye kitabu cha uzima. Unisafishe na udhalimu wote, unisaidie kuishi maisha ya utakatifu na kukuishia wewe sasa na hata milele. Namkataa shetani na kazi zake zote. Asante Bwana, kwa kunisamehe, asante Bwana kwa kunisafisha. Amen.

Hongera sana, baada ya kusema maneno hayo, sasa umeokoka. Tafuta kanisa lililo karibu nawe ambako utakutana na watu wanaohubiri wokovu wakuongoze katika njia inayofaa. Mungu akubariki sana.



No comments:

Post a Comment