Friday, November 2, 2012

ROHO MTAKATIFU NDANI YAO WAAMINIO

NEW

 
Fimbo ya musa ministry
Mafundisho ya neno la mungu
Somo: roho mtakatifu ndani yao waaminio
Mwl. Lukiko lukiko
NENO LA SOMO: MATENDO 1: 8a
Kwa watu waliookoka na kuamua kwa dhati kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ni mara nyingi sana utawasikia wakisema habari za Roho Mtakatifu. Na kwa wale ambao neema hii ya Roho Mtakatifu haijafunuliwa, kwao huona kuwa hakuna kitu kama hicho kinachoitwa Roho Mtakatifu na mara nyingi sana huwaona wale waliookoka na kujazwa Roho Mtakatifu kama wamechanganyikiwa.
Warumi 8:14, Biblia inasema; “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.” Maneno haya yanatufundisha mambo matatu muhimu.
1)    Kuongozwa.
Hii ina maana kuwa katika maisha ya mtu yeyote hapa duniani ni lazima kuna kuongozwa. Na kama kuna kuongozwa basi ni wazi kuwa kuna watu wawili wanahusika hapa. Mmoja ni Yule anayeongoza, na wingine ni Yule anayeongozwa. Hii inatupa picha kuwa kwa vyovyote vile mwanadamu hawezi kujiongoza mwenyewe ni lazima ategemee uongozi Fulani kutoka nje ya uwezo wake yeye mwenyewe. Sasa maandiko yametutajia kuwa kiongozi mmojawapo anayeweza kuwaongoza watu ni ROHO WA MUNGU.
Nafikiri sio vibaya nikisema kuwa kama Roho wa Mungu anaweza kuwaongoza watu, basi hata roho wa shetani naye anaweza kuwaongoza watu. Hawa ni viongozi wawili tofauti wenye sifa, uwezo, malengo, mbinu, na mwelekeo usiofanana katika ufundishaji wao. Ndio maana warumi 8:14 imetuambia kuwa matokeo ya kuongozwa na Roho wa Mungu ni kuwa mwana wa Mungu. Kwa maana hiyo wale wasioongozwa na Roho wa Mungu hao sio wana wa Mungu, na kama sio wana wa Mungu basi watakuwa wana wa shetani.
Swali: wewe unaongozwa na roho wa nani?
2)    Roho wa Mungu
Warumi 8: 14 inasema ‘wanaoongozwa na Roho wa Mungu’…. Ni vizuri sana tukajifunza japo kwa uchache kuhusu huyu anayeitwa Roho wa Mungu.
Matendo 1: 8 inasema “Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu,…” Luka 24:49 inasema “Tazama nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mijini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”
Roho Mtakatifu ni nini?
Maneno ya kitabu cha Luka yanatuambia kuwa mitume walitakiwa kuvikwa uwezo utokao juu kabla kutoka kwenda kuihubiri injili. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinatuambia kuwa Roho Mtakatifu angewajilia juu yao kabla ya kuanza kuihubiri injili. Matendo 2:1-5 “… Wote wakajazwa Roho Mtakatifu…”
Mtiririko huu wa maandiko unatupa kujua kuwa ule uwezo utokao juu ulionenwa kwenye kitabu cha Luka ilikuwa na maana ya kujazwa Roho Mtakatifu. Kwa maana hiyo tunaweza kusema sasa kuwa Roho Mtakatifu ni uwezo wa Mungu utokao juu mbinguni na kuwajaza wanadamu ili waweze kuishi sawasawa na mapenzi ya Mungu. Warumi 8: 14 imetuambia kuwa ‘wanaoongozwa na Roho wa Mungu hao ndio wana wa Mungu.’ Kwa maana hiyo Roho Mtakatifu ni kiongozi anayewaongoza watu katika kufanywa wana halisi wa Mungu.
Kwa mtu yeyote anayeokoka na kutaka kuishi maisha ya utakatifu na yenye kumpendeza Mungu, basi suala la kuwa na Roho wa Mungu ndani yake ni la muhimu sana. Ni vyema nikakuambia tangu mwanzo wa somo hili kuwa kuishi ndani ya wokovu bila kuwa na Roho Mtakatifu ni suala litakalokufanya usiingie mbinguni.
Warumi 8: 9 inasema “Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo huyo si wake.” Usipokuwa na Roho Mtakatifu ndani yako maandiko yanasema wewe si mtu wa kristo. Kwa maana hiyo wote walio watu wa kristo, na wana wa Mungu lazima wawe na Roho Mtakatifu ndani yao.
Roho Mtakatifu ni nafsi mojawapo katika Mungu mmoja. Huwezi ukazungumza habari Mungu, na Yesu kristo halafu ukamsahau Roho Mtakatifu. Huyu ndiye kiungo cha utendaji kazi wa Mungu. 1kor 12:3 insema ‘… wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Ni lazima uwe ndani ya Roho Mtakatifu ili uwe na uhalali wa kusema Yesu ni Bwana na kuweza kulitumia jina la Yesu.
Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipinga sana habari hizi za Roho mtakatifu, na wengine wanatuona sisi tuliojazwa Roho Mtakatifu kuwa tumechanganyikiwa. Lakini nikuambie siri moja kuwa Maisha ndani ya Yesu ni maisha ndani ya Roho Mtakatifu. Kama hauna maisha ndani ya Roho Mtakatifu basi jua hakika kuwa wewe huna maisha ndani ya Yesu na nikushauri tangu sasa anza kumwomba Mungu uwe na USHIRIKA NA ROHO MTAKATIFU.
NAWEZAJE KUMPOKEA ROHO MTAKATIFU
Kuna mambo kadhaa muhimu sana ya kuzingatia unapotaka kumpokea Roho Mtakatifu. Biblia inatoa mwongozo kwenye masuala kadhaa yanayokupa uwezo wa kujazwa Roho mtakatifu. Mambo yafuatayo ni muhimu kuyazingatia:
1)    Kuokoka na kuacha dhambi
Matendo 2:38 inasema hivi “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.” Maandiko haya yanatufunulia kuwa Roho Mtakatifu ni kipawa wanachopewa watu pale wanapotubu na kuamua kumpokea Yesu Kristo wawe Bwana na mwokozi wa maisha yao. Neno ‘kipawa’ Biblia za kiingereza zimelitaja kama ‘gift.’ Sasa ‘gift’ kwa Kiswahili linamaana ya ‘zawadi.’ Kwa maana hiyo Roho Mtakatifu ni zawadi ambayo Mungu huwapa wale waliompokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wao. Ndio maana yesu anasema ni ahadi ya Baba wa mbinguni kwa wale waaminio; Luka 24:49 ‘Na tazama nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu, lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu.’
Kila mtu anayeokoka ameahidiwa zawadi na Baba. Ahadi hii ni kuvikwa uwezo utokao juu, yaani kujazwa Roho Mtakatifu. Yesu mwenye alipobatizwa tu alijazwa Roho Mtakatifu pale pale mtoni. Mathayo 3:16 “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake.” Yesu kubatizwa haikuwa ina maaanisha kuwa alikuwa na dhambi, bali ilikuwa ni ishara kwetu kuwa tunahitaji kutakaswa.
Hebu tujiulizwe swali fupi. Ni kwa nini Roho wa Mungu alimshukia Yesu baada ya kubatizwa na si kabla ya hapo?
Jibu la swali hili linatokana na maneno ya Petro kwenye kitabu cha Matendo ya Mitume 2:38. Ilikuwa ni muhimu Roho Mtakatifu ashuke juu ya Yesu baada ya kubatizwa kwa sababu kwa utaratibu wa Mungu Roho wake hawezi kukaa mahali penye dhambi; hivyo yesu alitaka kutufundisha kuwa ili tuweze kumpokea Roho Mtakatifu ni lazima tutakaswe kwanza. Yeye ni MTAKATIFU na hivyo lazima akae mahali patakatifu.
Kwa maana hiyo hakuna mtu aliye nje ya wokovu au nje ya Kristo Yesu ambaye anaweza kujazwa Roho Mtakatifu. Matendo 10: 44-48, maandiko yanazungumza kuhusu watu wa mataifa (kwa lugha nyingine, wale ambao walikuwa hawajaokoka) ambao walimwagiwa kipawa ch Roho Mtakatifu, lakini ilimbidi Petro kuwabatiza japo walikuwa wameshukiwa na Roho wa Mungu. Maana yake ni kuwa ili ukae vizuri na Roho Mtakatifu ni lazima utakswe na kufutwa dhambi zako zote.
2)    Kuomba ujazo wa Roho Mtakatifu juu yako
Unapokwisha kutubu na kuokoka inabidi uombe ili Roho wa Mungu aje juu yako. Kuna njia mbili za maombi ya kujazwa Roho Mtakatifu.
Ø Kuomba mwenyewe
Ukishaokoka unaweza kuchukua hatua ya imani na ukaomba mwenyewe ili ujazwe Roho Mtakatifu. Kitabu cha Luka 3:21-22 imeandikwa hivi “Ikawa watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake…” Hapa tunaona kuwa Yesu baada ya kubatizwa alichukua hatua ya kuomba mwenyewe, na alipokuwa katika kuomba ndipo mbingu zikamfunukia Roho Mtakatifu akaja juu yake.
Luka 11:13 imeandikwa hivi; “Basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba yenu wa mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” Maneno haya yanatufundisha kuwa ujazo wa Roho Mtakatifu ni kipawa unachoweza kukiomba kwa Baba wa mbinguni. Unauhuru wa kimaandiko kusimama mwenyewe na kujiombea ujazwe Roho Mtakatifu.
Ø Kuombewa na watumishi waliopakwa mafuta
Mungu ameweka utaratibu wa watu kujazwa Roho Mtakatifu kwa kuombewa na watumishi wa Mungu waliopakwa mafuta kwa huduma ya Roho Mtakatifu. Matendo 19:1-7, inatuonyesha kuwa kubatizwa bila kumpokea Roho Mtakatifu haitoshi kukukamilisha kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Paulo aliwakuta watu ambao tayari walishabatizwa kwa maji, lakini hawakujazwa Roho Mtakatifu. Paulo anawauliza; Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?
Ni swali ambalo linamhusu kila mtu anayeamua kumfuata Yesu Kristo. Hebu na wewe jiulize swali hili; je ulipokea Roho Mtakatifu ulipoamini? Watu wa kipindi kile cha akina Paulo walijibu wakasema hata kusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu hatujawahi. Leo hii wengi sana tumesikia habari za Roho Mtakatifu lakini ni wachache sana ambao wamejazwa Roho Mtakatifu na wanatembea naye.
FAIDA ZA KUJAZWA ROHO MTAKATIFU
Kuna mambo mengi sana katika ulimwengu wa roho ambayo yanategemea sana uwepo wa Roho Mtakatifu. Suala la maombi, kuishi maisha matakatifu, nguvu za rohoni na kumtumikia Mungu katika roho na kweli ni mambo ambayo yanahitaji Roho wa Mungu awepo ndani ya mtu ili kumwezesha kuyafanya. Faida za kumpokea Roho Mtakatifu ni kama zifuatazo:
*    Roho Mtakatifu ni uwezo wa Mungu unaomwezesha mtu kuishi maisha ya ushindi katika wokovu.
Matendo 4:31 inasema: “Hata walipokwisha kumwomba Mungu mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu wakanena neno la Mungu kwa Ujasiri.” Mitume kabla ya kujazwa Roho Mtakatifu hawakuwa na ujasiri wa kumkiri na kumtangaza Yesu Kristo, lakini walipokwisha kujazwa Roho hakuna mtu aliyeweza kuwazuia wasiieneze injili.
Luka 24:49 insema ‘… kaeni humu mjini hata mvikwe uwezo utokao juu.” Roho Mtakatifu ni uwezo utokao juu kwa Mungu kwa ajili kuimarisha watu wake. Usipokuwa naye Roho maana yake hauna uweza wa Mungu ndani yako wa kukuwezesha kuishi kwa ushindi.
Watu wote waliojazwa Roho Mtakatifu ni watu wa ushindi daima. Katika Matendo ya mitume watu wa sinagogi la mahuru na wengine wengi walishindana na Stefano ‘lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.’ushindi wa mkristo yeyote Yule unatagemea sana nguvu za Roho Mtakatifu zilizo ndani yake.
*    Roho Mtakatifu anatufundisha kweli na atakupasha habari za mambo yanayokuja
Yohana 14:25-26, Yohana 16:13
Mistari hii inatupa kujua kuwa tuna uwezo wa kujifunza kweli yote kwa mwongozo wa Roho Mtakatifu na kuyajua mambo yajayo ikiwa tutakubali Roho wa Mungu atuongoze. 1Kor 2:10 inasema ‘Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote hata mafunbo ya Mungu.’ Tunaweza kuyajua mambo yote kwa kufunuliwa na Roho na ili hii itokee ni lazima uwe umejazwa Roho Mtakatifu.

2 comments: