NEW
Fimbo ya musa
ministry
Mafundisho ya
neno la mungu
Somo: roho mtakatifu ndani yao waaminio
Mwl.
Lukiko lukiko
NENO LA SOMO: MATENDO 1: 8a
Kwa
watu waliookoka na kuamua kwa dhati kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ni mara
nyingi sana utawasikia wakisema habari za Roho Mtakatifu. Na kwa wale ambao
neema hii ya Roho Mtakatifu haijafunuliwa, kwao huona kuwa hakuna kitu kama
hicho kinachoitwa Roho Mtakatifu na mara nyingi sana huwaona wale waliookoka na
kujazwa Roho Mtakatifu kama wamechanganyikiwa.
Warumi
8:14, Biblia inasema; “Kwa kuwa wote wanaoongozwa
na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.” Maneno haya yanatufundisha mambo
matatu muhimu.
1) Kuongozwa.
Hii
ina maana kuwa katika maisha ya mtu yeyote hapa duniani ni lazima kuna
kuongozwa. Na kama kuna kuongozwa basi ni wazi kuwa kuna watu wawili wanahusika
hapa. Mmoja ni Yule anayeongoza, na wingine ni Yule anayeongozwa. Hii inatupa
picha kuwa kwa vyovyote vile mwanadamu hawezi kujiongoza mwenyewe ni lazima
ategemee uongozi Fulani kutoka nje ya uwezo wake yeye mwenyewe. Sasa maandiko
yametutajia kuwa kiongozi mmojawapo anayeweza kuwaongoza watu ni ROHO WA MUNGU.
Nafikiri
sio vibaya nikisema kuwa kama Roho wa Mungu anaweza kuwaongoza watu, basi hata
roho wa shetani naye anaweza kuwaongoza watu. Hawa ni viongozi wawili tofauti
wenye sifa, uwezo, malengo, mbinu, na mwelekeo usiofanana katika ufundishaji
wao. Ndio maana warumi 8:14
imetuambia kuwa matokeo ya kuongozwa na Roho wa Mungu ni kuwa mwana wa Mungu.
Kwa maana hiyo wale wasioongozwa na Roho wa Mungu hao sio wana wa Mungu, na
kama sio wana wa Mungu basi watakuwa wana wa shetani.
Swali:
wewe unaongozwa na roho wa nani?
2) Roho wa Mungu
Warumi
8: 14 inasema ‘wanaoongozwa na Roho wa
Mungu’…. Ni vizuri sana tukajifunza japo kwa uchache kuhusu huyu anayeitwa
Roho wa Mungu.
Matendo
1: 8 inasema “Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu,…” Luka 24:49 inasema
“Tazama nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mijini, hata mvikwe uwezo utokao juu.”
Roho
Mtakatifu ni nini?
Maneno
ya kitabu cha Luka yanatuambia kuwa mitume walitakiwa kuvikwa uwezo utokao juu
kabla kutoka kwenda kuihubiri injili. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinatuambia
kuwa Roho Mtakatifu angewajilia juu yao kabla ya kuanza kuihubiri injili.
Matendo 2:1-5 “… Wote wakajazwa Roho Mtakatifu…”
Mtiririko
huu wa maandiko unatupa kujua kuwa ule uwezo
utokao juu ulionenwa kwenye kitabu cha Luka ilikuwa na maana ya kujazwa Roho Mtakatifu. Kwa maana hiyo tunaweza
kusema sasa kuwa Roho Mtakatifu ni uwezo wa Mungu utokao juu mbinguni na
kuwajaza wanadamu ili waweze kuishi sawasawa na mapenzi ya Mungu. Warumi 8: 14
imetuambia kuwa ‘wanaoongozwa na Roho wa Mungu hao ndio wana wa Mungu.’ Kwa
maana hiyo Roho Mtakatifu ni kiongozi anayewaongoza watu katika kufanywa wana
halisi wa Mungu.
Kwa
mtu yeyote anayeokoka na kutaka kuishi maisha ya utakatifu na yenye kumpendeza
Mungu, basi suala la kuwa na Roho wa Mungu ndani yake ni la muhimu sana. Ni
vyema nikakuambia tangu mwanzo wa somo hili kuwa kuishi ndani ya wokovu bila kuwa na Roho Mtakatifu ni suala
litakalokufanya usiingie mbinguni.
Warumi
8: 9 inasema “Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo huyo si wake.”
Usipokuwa na Roho Mtakatifu ndani yako maandiko yanasema wewe si mtu wa kristo.
Kwa maana hiyo wote walio watu wa kristo, na wana wa Mungu lazima wawe na Roho
Mtakatifu ndani yao.
Roho
Mtakatifu ni nafsi mojawapo katika Mungu mmoja. Huwezi ukazungumza habari
Mungu, na Yesu kristo halafu ukamsahau Roho Mtakatifu. Huyu ndiye kiungo cha
utendaji kazi wa Mungu. 1kor 12:3 insema ‘… wala hawezi mtu kusema, Yesu ni
Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Ni lazima uwe ndani ya Roho Mtakatifu
ili uwe na uhalali wa kusema Yesu ni Bwana na kuweza kulitumia jina la Yesu.
Kuna
baadhi ya watu wamekuwa wakipinga sana habari hizi za Roho mtakatifu, na
wengine wanatuona sisi tuliojazwa Roho Mtakatifu kuwa tumechanganyikiwa. Lakini
nikuambie siri moja kuwa Maisha ndani ya
Yesu ni maisha ndani ya Roho Mtakatifu. Kama hauna maisha ndani ya Roho
Mtakatifu basi jua hakika kuwa wewe huna maisha ndani ya Yesu na nikushauri
tangu sasa anza kumwomba Mungu uwe na USHIRIKA NA ROHO MTAKATIFU.
NAWEZAJE
KUMPOKEA ROHO MTAKATIFU
Kuna
mambo kadhaa muhimu sana ya kuzingatia unapotaka kumpokea Roho Mtakatifu.
Biblia inatoa mwongozo kwenye masuala kadhaa yanayokupa uwezo wa kujazwa Roho
mtakatifu. Mambo yafuatayo ni muhimu kuyazingatia:
1) Kuokoka na kuacha dhambi
Matendo
2:38 inasema hivi “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo,
mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.” Maandiko
haya yanatufunulia kuwa Roho Mtakatifu ni kipawa wanachopewa watu pale
wanapotubu na kuamua kumpokea Yesu Kristo wawe Bwana na mwokozi wa maisha yao.
Neno ‘kipawa’ Biblia za kiingereza zimelitaja kama ‘gift.’ Sasa ‘gift’ kwa
Kiswahili linamaana ya ‘zawadi.’ Kwa maana hiyo Roho Mtakatifu ni zawadi ambayo
Mungu huwapa wale waliompokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wao. Ndio maana yesu
anasema ni ahadi ya Baba wa mbinguni kwa wale waaminio; Luka 24:49 ‘Na tazama
nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu, lakini kaeni humu mjini, hata
mvikwe uwezo utokao juu.’
Kila
mtu anayeokoka ameahidiwa zawadi na Baba. Ahadi hii ni kuvikwa uwezo utokao
juu, yaani kujazwa Roho Mtakatifu. Yesu mwenye alipobatizwa tu alijazwa Roho
Mtakatifu pale pale mtoni. Mathayo 3:16 “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara
akapanda kutoka majini; na tazama mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija
juu yake.” Yesu kubatizwa haikuwa ina maaanisha kuwa alikuwa na dhambi, bali
ilikuwa ni ishara kwetu kuwa tunahitaji kutakaswa.
Hebu
tujiulizwe swali fupi. Ni kwa nini Roho wa Mungu alimshukia Yesu baada ya
kubatizwa na si kabla ya hapo?
Jibu
la swali hili linatokana na maneno ya Petro kwenye kitabu cha Matendo ya Mitume
2:38. Ilikuwa ni muhimu Roho Mtakatifu ashuke juu ya Yesu baada ya kubatizwa
kwa sababu kwa utaratibu wa Mungu Roho wake hawezi kukaa mahali penye dhambi;
hivyo yesu alitaka kutufundisha kuwa ili tuweze kumpokea Roho Mtakatifu ni
lazima tutakaswe kwanza. Yeye ni MTAKATIFU na hivyo lazima akae mahali
patakatifu.
Kwa
maana hiyo hakuna mtu aliye nje ya wokovu au nje ya Kristo Yesu ambaye anaweza
kujazwa Roho Mtakatifu. Matendo 10: 44-48, maandiko yanazungumza kuhusu watu wa
mataifa (kwa lugha nyingine, wale ambao walikuwa hawajaokoka) ambao walimwagiwa
kipawa ch Roho Mtakatifu, lakini ilimbidi Petro kuwabatiza japo walikuwa
wameshukiwa na Roho wa Mungu. Maana yake ni kuwa ili ukae vizuri na Roho
Mtakatifu ni lazima utakswe na kufutwa dhambi zako zote.
2) Kuomba ujazo wa Roho Mtakatifu juu
yako
Unapokwisha
kutubu na kuokoka inabidi uombe ili Roho wa Mungu aje juu yako. Kuna njia mbili
za maombi ya kujazwa Roho Mtakatifu.
Ø Kuomba
mwenyewe
Ukishaokoka
unaweza kuchukua hatua ya imani na ukaomba mwenyewe ili ujazwe Roho Mtakatifu.
Kitabu cha Luka 3:21-22 imeandikwa hivi “Ikawa watu wote walipokwisha
kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye
anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake…” Hapa tunaona
kuwa Yesu baada ya kubatizwa alichukua hatua ya kuomba mwenyewe, na alipokuwa
katika kuomba ndipo mbingu zikamfunukia Roho Mtakatifu akaja juu yake.
Luka
11:13 imeandikwa hivi; “Basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu
vipawa vyema, je! Baba yenu wa mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?” Maneno haya yanatufundisha
kuwa ujazo wa Roho Mtakatifu ni kipawa unachoweza kukiomba kwa Baba wa
mbinguni. Unauhuru wa kimaandiko kusimama mwenyewe na kujiombea ujazwe Roho
Mtakatifu.
Ø Kuombewa
na watumishi waliopakwa mafuta
Mungu
ameweka utaratibu wa watu kujazwa Roho Mtakatifu kwa kuombewa na watumishi wa
Mungu waliopakwa mafuta kwa huduma ya Roho Mtakatifu. Matendo 19:1-7,
inatuonyesha kuwa kubatizwa bila kumpokea Roho Mtakatifu haitoshi kukukamilisha
kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Paulo aliwakuta watu ambao tayari walishabatizwa
kwa maji, lakini hawakujazwa Roho Mtakatifu. Paulo anawauliza; Je! Mlipokea Roho Mtakatifu
mlipoamini?
Ni
swali ambalo linamhusu kila mtu anayeamua kumfuata Yesu Kristo. Hebu na wewe
jiulize swali hili; je ulipokea Roho Mtakatifu ulipoamini? Watu wa kipindi kile
cha akina Paulo walijibu wakasema hata kusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu
hatujawahi. Leo hii wengi sana tumesikia habari za Roho Mtakatifu lakini ni
wachache sana ambao wamejazwa Roho Mtakatifu na wanatembea naye.
FAIDA
ZA KUJAZWA ROHO MTAKATIFU
Kuna
mambo mengi sana katika ulimwengu wa roho ambayo yanategemea sana uwepo wa Roho
Mtakatifu. Suala la maombi, kuishi maisha matakatifu, nguvu za rohoni na
kumtumikia Mungu katika roho na kweli ni mambo ambayo yanahitaji Roho wa Mungu
awepo ndani ya mtu ili kumwezesha kuyafanya. Faida za kumpokea Roho Mtakatifu
ni kama zifuatazo:
Roho
Mtakatifu ni uwezo wa Mungu unaomwezesha mtu kuishi maisha ya ushindi katika
wokovu.
Matendo
4:31 inasema: “Hata walipokwisha kumwomba Mungu mahali pale walipokusanyika
pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu wakanena neno la Mungu kwa Ujasiri.”
Mitume kabla ya kujazwa Roho Mtakatifu hawakuwa na ujasiri wa kumkiri na
kumtangaza Yesu Kristo, lakini walipokwisha kujazwa Roho hakuna mtu aliyeweza
kuwazuia wasiieneze injili.
Luka
24:49 insema ‘… kaeni humu mjini hata mvikwe uwezo utokao juu.” Roho Mtakatifu
ni uwezo utokao juu kwa Mungu kwa ajili kuimarisha watu wake. Usipokuwa naye
Roho maana yake hauna uweza wa Mungu ndani yako wa kukuwezesha kuishi kwa
ushindi.
Watu
wote waliojazwa Roho Mtakatifu ni watu wa ushindi daima. Katika Matendo ya
mitume watu wa sinagogi la mahuru na wengine wengi walishindana na Stefano
‘lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema
naye.’ushindi wa mkristo yeyote Yule unatagemea sana nguvu za Roho Mtakatifu
zilizo ndani yake.
Roho
Mtakatifu anatufundisha kweli na atakupasha habari za mambo yanayokuja
Yohana
14:25-26, Yohana 16:13
Mistari
hii inatupa kujua kuwa tuna uwezo wa kujifunza kweli yote kwa mwongozo wa Roho
Mtakatifu na kuyajua mambo yajayo ikiwa tutakubali Roho wa Mungu atuongoze. 1Kor
2:10 inasema ‘Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza
yote hata mafunbo ya Mungu.’ Tunaweza kuyajua mambo yote kwa kufunuliwa na Roho
na ili hii itokee ni lazima uwe umejazwa Roho Mtakatifu.
that is great! God bless u!
ReplyDeleteCONGRATULATIONS!
ReplyDeleteIt's a good work, keep it up...