Thursday, November 20, 2014

ISAIDIE ROHO YAKO KUUSHINDA MWILI WAKO (SEHEMU YA 1)

Our Daily Mana


UTANGULIZI

Hili ni somo linalohusu namna mwanadamu anavyotakiwa kufanya ili aweze kumshinda Ibilisi, mchakato huu wa kumshinda Ibilisi ni mkubwa na mgumu ambao huhusisha sehemu zote za mwili yaani roho, nafsi na mwili. Roho ndiyo sehemu ya mwili ambayo huhitaji kujazwa nguvu ya Mungu ili iweze kuushinda mwili ambao ni wa dunia hii, mwili ambao nia yake ni uharibifu kama tutakavyoona katika somo hili. 

Mwanadamu anakuwa na roho ambayo huwa kama imezimia au haifanyi kazi ipasavyo pale ambapo anakuwa ameshikwa na maovu na kutokumtumikia Mungu, wakati huu roho hii hujazwa na roho chafu ambazo haziendani na mapenzi ya Mungu kwa maana hazitokani na Mungu. Akisha kumpokea Yesu mtu huyu hujiwa na Roho Mtakatifu ambaye kwa kutegemea na jinsi huyu mtu anavyojiweka karibu na Mungu ndivyo huendelea kukua na kujijenga, mtu huyu huanza kumshinda shetani na kuuzuia mwili wake kutenda dhambi. 

Katika somo hili tunaangalia jinsi ambavyo mtu anaweza kuisaidia roho yake kukuzwa na Roho Mtakatifu na kuushinda mwili na kutoa mwanga pia juu ya hasara ambayo mtu ambaye hajaokoka anakuwa nayo kwa kutokuwa na Roho Mtakatifu. Ushauri  unatolewa mwishoni namna ambavyo mtu anaweza kutumia vitu na mambo kadhaa kuitia roho yake uwezo wa kimungu ili aweze kuishinda dhambi inayokaa mwilini mwake.
Wagalatia 5:17
Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho hushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.
Warumi 8:5-8
5 Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. 6 Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani. 7 Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. 8 Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu.



Ni wazi kwamba mwili hushindana na roho, na daima hivi vimepingana na haviwezi kupatana. Hivyo mpendwa unatakiwa kuwa na nguvu nyingi za roho ili roho ipate kuwa na nguvu za kutosha za kuushinda mwili. Kwani kwa kawaida kama unaulisha mwili kila siku halafu roho huilishi, matokeo ni kwamba mwili utapata nguvu zaidi kuliko roho na itakuwa vigumu kwako kushinda. Vitu unavyovijua kuhusu Mungu vyaweza kuwa katika akili lakini kawaida ni kwamba kama roho isipokuwa na kawaida ya kuvila vyakula hivyo kamwe haiwezi kuimarika. 

Kuweka neno la Mungu akilini ni jambo lingine na kulihamishia katika roho yako na kuliishi ni kazi nyingine. Maarifa yaliyo katika akili yasipohamishiwa rohoni kwa njia ya maombi ni sawa na kuwa na chakula halafu usipike, hakiwezi kwenda tumboni na kitabaki stoo na utakufa na njaa kama yule ambaye hana chakula. Ndiyo maana Mungu anasema katika kitabu cha Yoshua 1:8 “Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo;…” maneno hayo ya mwisho yanasisitiza kwamba mtu haitoshi tu kwake kuyatafakari maneno ya Mungu bali pia aangalie kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo. 

Hii inaonesha kuwa kuyajua na kuyafahamu maneno ya Mungu ni kitu kingine na kutenda au kuyaweka yale uliyoyasoma katika matendo pia ni suala lingine. Tukisha kuyatenga hayo mambo mawili ndipo tutakuja kutofautisha kwamba kuna mtu anayelijua neno halafu halifanyii kazi na kuna mtu ambaye analijua na analifanyia kazi. Kulifanyia kazi hapa inamaanisha kuishi sawasawa na neno hilo, ndiyo maana kuna shetani Ibilisi ambaye yumkini analijua neno la Mungu kuliko watumishi wengi kama sio wote wa Mungu lakini haliishi hilo neno na badala yake analitumia kuwatega na kuwaangusha watumishi wa Mungu na hadi wakati mwingine alijaribu kumuangusha Kristo mwenyewe akitumia neno. Soma Mathayo sura ya nne.

 Hivyo kulijua neno na kujua biblia pekee haitoshi kama hautatumia juhudi za kulileta neno hilo katika matendo. Uwezo wa kulileta neno katika matendo huanzia katika roho kabla haujaja katika mwili, ndiyo maana watu wanaojishughulisha sana na maombi ndio wenye uwezekano mkubwa sana wa kuwa katika mapenzi ya mungu na matendo mema kuliko wale ambao hawakai katika maombi, maombi na maisha matakatifu ni vitu vinavyoenda pamoja na kamwe huwezi kuvitenganisha, ukianza kuvipambanua utagundua kuwa yale tunayofundishwa na kutamani kumfanyia Mungu katika maisha yetu, humeng’enywa na kuja kutendwa katika maisha yetu na sisi kupata nguvu ya kuyatekeleza kupitia maombi. 

Yesu siyo kwamba hakujua kwamba Mungu yupo, alijua sana, siyo kwamba hakujua kuwa hakutakiwa kutenda dhambi, alifahamu sana. Siyo kwamba hakujua kwamba alitakiwa kukamilisha yale aliyotumwa kuja kuyatekeleza duniani, alifahamu sana, lakini pale ambapo nguvu ya mwili ilizidi nguvu yake ya Roho alithubutu kuomba kikombe kimuepuke. Akilitambua hilo, Kristo aliendelea kuomba hadi akalitimiliza kusudi la Mungu. Hata katika kila huduma alizokuwa anafanya alikuwa anaomba kwanza, siyo kwamba alikuwa hajui namna ya kuyaamuru mapepo yatoke, au alikuwa hajui kuwa mapepo hayana mamlaka mbele yake, alikuwa anajua elimu yote, isipokuwa alikuwa anahitaji maombi ili yauweke ujuzi alionao katika matumizi kama ambavyo tumbo hukiweka chakula katika mfumo au namna inayofaa kutumiwa na mwili. 
1Petro 3:18
Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa.
Ndiyo, Bwana Yesu hakuuonea huruma mwili wake, akakubali kuutesa kwa kuutiisha chini ya mapenzi ya Mungu na tunaona kuwa kwa kutokuuzingatia mwili alipata faida ya kuukomboa ulimwengu mzima na kile alichotumwa na Baba aliweza kukikamilisha.

Mtu anapookoka roho yake inaanza kuishi ndani yake-inakuwa imebadilishwa kutoka kumilikiwa na roho wachafu, na kuanza kumilikiwa na Roho Mtakatifu ambapo roho hii huendelea kuimarika siku hadi siku, ikikua kama mtoto aliyezaliwa. Roho hii inakuwa ni kama mtoto mdogo ambaye hajui vitu. Kama mtoto mdogo asivyofanya mambo yaliyo na maana mbele ya wakubwa, roho hii pia katika hatua za awali huwa na tabia hizo, kwa mfano ni kawaida kumuona mtu aliyeokoka juzijuzi akiimba nyimbo za bongo flava na kufanya mambo mengine mengi ambayo hayaoneshi ukomavu mzuri wa kiroho. 

Hapa nitoe ushuhuda mmoja kuhusu dada yangu mmoja niliyekuwa namlea kiroho, wakati tunafahamiana huyu dada alikuwa ana mazoea ya kuvaa suruali zinazobana sana na suala la kuvaa suruali kwake lilikuwa kawaida. Na mimi nilianza kumuhoji juu ya maisha yake binafsi na jinsi anavyomtumikia Mungu. Kwa sababu siku zote huwa naamini katika kanuni hii ambayo niliiandika katika lugha ya kiingereza “Put  your focus on one’s spiritual weakness to address it, after you have addressed it, outward weakness will be addressed by default,” kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba tazama udhaifu wa mtu wa rohoni, ukiisha kuuondoa huo, udhaifu wa nje utakuwa umeshaondoka pia.

 Niligundua kuwa yule dada alikuwa hana mazoea ya kibinafsi ya kufunga na kumtafuta Mungu. Kwa hiyo mahusiano yake binafsi na Mungu hayakuwa yamekomaa sana. Roho yake ilikuwa dhaifu sana na hivyo hakukuwa na nguvu itokayo ndani ya kumsaidia kuushinda mwili wake kwani Roho yake ilikuwa bado inakaliwa na baadhi ya roho zilizokuwa haziendani na kusudi la Mungu kwani alikuwa bado mchanga rohoni mwake. Ndipo nilipoanza kumsihi aanze kufunga na kuomba.

Aliniambia kuwa alikuwa na vidonda vya tumbo nami nikamwambia aanze kwa kufunga kwa masaa machache, baadaye aliweza kufunga na akawa anafanya maombi ya fellowship na maombi yake binafsi.

Baada ya kupita muda sikumuona tena yule binti akivaa suruali, baada ya kuja kumuuliza aliniambia alikuwa akivaa suruali anajiona yuko uchi! Hapa ndipo nilipogundua kuwa roho yake tayari ilishakuwa na nguvu ya kutosha na tayari nguvu iliyo ndani ya roho yake ilishaushinda mwili na roho zile chafu ndani yake zilishaondoka kabisa.

Nilikaa na jamaa yangu mwingine ambaye hajashuhudia mambo mengi ya kiroho akileta changamoto juu ya kunena kwa lugha akiwa haamini katika hilo akihoji kwa nini yeye haneni kwa lugha, nikamwambia aendelee kumtafuta Mungu kwa bidii maana kiwango chake hakijafikia uwezo huo. Akaonekana kutokuamini hilo lakini nikagundua kuwa bado kutokuamini kwake kunaletwa na ule uchanga wa kiroho.

Mtu huwa hajui mambo mengi na wakati mwingine kubishana na watu kuhusu mambo kadhaa ya Mungu  kwa maana  roho yake haina mafundisho ya kutosha na hii(roho) huwa na tabia zote za mtoto mchanga kwani haiwezi vizuri kupambanua na vitu vinavyoingia ndani yake wakati huu hushikwa sana na uangalizi mkubwa sana unatakiwa katika malezi ya roho hii kwani mambo yatakayopandikizwa katika hatua hii ndiyo yatakuwa msingi wa maisha katika kiumbe hicho kipya.

Roho hii inakuwa na tabia kama za mwili wa mwanadamu kwa misingi kwamba itakuwa inahitaji kifungua kinywa, lanchi na dina(chakula) kama mwili, usipoilisha roho hii itadhoofika na ikishadhoofika, mwili uta ‘take over’, ndiyo maana yesu akasema roho I radhi mwili ni dhaifu. Na alihitaji kuwa mwombaji sana, akafunga siku nyingi ili kuudhoofisha mwili na kuiimarisha roho.

Roho ndiyo ibebayo mapenzi ya Mungu, mwili ni wa dunia hivyo hauielewi kabisa roho pale ambapo roho hiyo inakuwa inafanya kila aina ya kampeni kumpendeza Mungu. Ndiyo maana Paulo anasema katika Warumi 8:13 kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.

Kwa kuyafuata mambo ya mwili mwanadamu hujiweka katika hatari ya mauti kwani kwa kuwa mwili ni wa dunia hii wenyewe hutamani tu mambo ya dunia ambayo yamekatazwa na Mungu na matokeo yake ni uadui na Mungu na mtu huyu anayeufuata mwili kwa kuwa anaenda kinyume na mapenzi ya Mungu huishia kwenye mauti kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti. Kitu chochote utakachofanya kitakachoiimarisha roho yako ni muhimu kukifanya kwa bidii zote na usipofanya hivyo utabaki kutamani tu kuwa na kiwango fulani cha huduma na kushindwa kukifikia kwani roho yako haijashiba vya kutosha kufika huko.


1 comment: