Mwanadamu anakuwa na roho ambayo huwa kama imezimia au haifanyi kazi ipasavyo pale ambapo anakuwa ameshikwa na maovu na kutokumtumikia Mungu, wakati huu roho hii hujazwa na roho chafu ambazo haziendani na mapenzi ya Mungu kwa maana hazitokani na Mungu. Akisha kumpokea Yesu mtu huyu hujiwa na Roho Mtakatifu ambaye kwa kutegemea na jinsi huyu mtu anavyojiweka karibu na Mungu ndivyo huendelea kukua na kujijenga, mtu huyu huanza kumshinda shetani na kuuzuia mwili wake kutenda dhambi.
Karibu katika sehemu ya pili ya somo hili, tutazame pamoja mambo ambayo husaidia kuijengea mazingira roho yako kukua.
Vyakula vya kiroho ni hivi vifuatavyo:
1.
Maombi
2.
Neno la Mungu
3.
Nyimbo za kumsifu na kumtukuza Mungu
4.
Tafakari na mawazo juu ya Mungu na
matendo yake makuu.
Mambo ambayo husaidia kuijengea
mazingira roho yako kukua
Kuna
mambo katika maisha ambayo kwa kawaida mwanadamu anayafanya, lakini
nikufahamishe leo kuwa katika mambo yote unayoyafanya yana athari katika
ulimwengu wa roho na makuzi ya roho yako yanategemea moja kwa moja mambo hayo,
hebu sasa tuangalie baadhi ya mambo ambayo yanaweza kukusaidia kuikuza roho
yako.
1. Vitu
unavyopenda kuangalia.
Zaburi 119:37 “Unigeuze macho yangu
nisitazame visivyofaa, unihuishe katika njia yako.”
Kuna vitu ambavyo havifai kama Daudi
anavyosema ambavyo vitajaa ndani ya nafsi yako kama ukiendelea kuviangalia,
picha za uchi, matendo ya kikatili na matusi. Kimsingi vitu ambavyo havikupi
kuongezeka kimaarifa na wala haviisaidii roho yako kukua siyo vizuri
kuviangalia. Mtu mmoja kaniuliza swali, “Kwani kuna maasi gani kwa mimi
kuangalia mziki wa bongo flava?” na mimi nikamuuliza, kwani Napata nini cha
zaidi ambacho ni cha faida kwa kuangalia hayo? Kimsingi vitu hivi, kabla
hatujazama ndani zaidi vinatumiwa tu kumsahaulisha mtu majukumu yake na
kumchelewesha. Suala siyo kupata burudani, kwani Mungu hutuburudisha na ziko
burudani nyingi zenye utukufu wa Mungu ambazo tunaweza kuzitumia badala ya kila
saa kukubali kuburudishwa na watu ambao hawana hofu au imani tuliyonayo sisi.
Vipo vitu vya msingi ambavyo waweza
kuviangalia na visikudhuru, lakini uwe makini kuna wakati baadhi ya vitu
vinaweza kuwa havina athari ya moja kwa moja katika maisha yako ya kiroho
lakini vikakuchukulia muda wako mwingi sana kuliko muda wa kusoma neno la Mungu
na kuomba.
Vitu hivyo ni kama muvi na mpira na
vilevile kucheza gemu. Ni kweli kwamba kuna wakati ambao mtu huhitaji kupumzika
na kujiburudisha kidogo baada ya kazi, wala hapa sikusudii kuwapiga marufuku
watu kufanya vitu hivi, lengo langu hapa ni kukutahadharisha tu kuwa kama
ambavyo vitu hivi vinaweza kukuchelewesha kupika na kusababisha ukaahirisha
kula chakula cha kimwili, vilevile vinaweza kukuharibia ratiba yako ya kuilisha
roho yako. Hivyo unapoviangalia hivi hakikisha kuwa haviathiri ratiba yako ya
kwenye maombi wala ya kusoma biblia.
Anaposema Daudi kwamba anaomba kuhuishwa
katika njia ya Mungu anamaanisha nini? Anataka kujizoeza kuviangalia vitu
ambavyo vitamkuza katika maisha yake ya rohoni. Angalia sana ni vitu gani
unavyovitilia maanani katika maisha yako ili usije ukapotea.
2.
Vitu
unavyovisikiliza mara kwa mara
2korintho15:33.
“Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu
tabia njema.”
Kile unachopenda kukisikiliza kama ni kibaya, katika
mazungumzo na rafiki zako, tabia yako itaendana na yale mazungumzo. Nakumbuka
nikiwa mdogo nilichelewa sana kuzifahamu habari za mapenzi na wasichana kwa
sababu rafiki zangu walikuwa hawaziongelei kabisa, ulipofika muda wa kubalehe
mimi nilikuwa nina tabia ya kujitenga na kila aliyekuwa anapenda habari hizo,
nikawa na tabia njema lakini baadaye nilipopata marafiki wapya ambao walikuwa
wanapenda sana habari hizo, nilijikuta naharibikiwa na kuingia kwenye tabia
hiyo mbaya kama nini sijui!
Ndiyo maana wapendwa wenye watoto
mnapaswa kuwaangalia sana kuhusu marafiki gani wanaokuwa nao muda mwingi,
yumkini mzazi wangu angekuwa makini katika hilo angeniondoa pale nilipokuwa
nimetumbukia enzi hizo. Lakini simlaumu, kwa kuwa hakujua.
3. Vitu
unavyopenda kuviongea mara kwa mara.
Zaburi 141:3
“Ee Bwana, uweke
mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.”
Daudi anamuomba Mungu aweke mngojezi mlangoni
pa midomo yake ili aweze kuongea mambo yenye utukufu mbele za Mungu. Kile
unachokisema mtumishi wa Mungu kinasaidia sana katika kuamua kwamba wewe ni mtu
wa Mungu na kukutambulisha kwa wengine kama umeokoka kweli, basi kama mtumishi
wa Mungu unapenda kunena maneno machafu yanayopelekea watu wengine kuumia utasababisha
magomvi na kujikosesha amani hali ambayo itasababisha ushindwe kusoma neno wala
kuomba kwa sababu moyo wako saa zote umekwazika na hauna amani.
Marko 7:20
“Akasema,
Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi.”
Ni afadhali unaposikia maneno yanayokukwaza
ukanyamaza kuliko kuongea katika hasira kwani maneno unayoyatoa yanaweza
kuzidisha magomvi.
Biblia imetoa maonyo mengi sana kuhusu maneno
na kumuhimiza mtu wa Mungu kuwa na maneno machache, awe mwepesi wa kusikia
lakini asiwe mwepesi wa kuongea, mahali hapa pasingetosha kujadili athari za
ulimi kwani ni mambo mengi sana yanayohusiana nao ambayo tungepaswa kuyapitia.
Cha msingi hapa tu ni kuwa makini na kumuomba Mungu ili yale tunayoyasema na
kuwaambia watu yawe yamekolea munyu, yaonye, yafundishe, yatie moyo na
kuendeleza upendo na msamaha.
Kolosai 4:6
“Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua
jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.”
4.
Vitu
vilivyo moyoni mwako.
Zaburi 119:11
Moyoni mwangu nimeliweka neno
lako, Nisije nikakutenda dhambi.
Daudi ana kitu alichokiweka ndani ya moyo wake ambacho kinamsaidia
kuishi sawasawa na mapenzi ya Mungu, kwanini Daudi ameliweka neno la Mungu
moyoni, na siyo mahali pengine? Ni kwa sababu moyo ndiyo huwa chanzo cha uzima
na chanzo cha mauti, kilicho moyoni ndicho hutoka moja kwa moja na kuathiri
maisha ya mtu.
Jeremiah 17:9 Moyo huwa mdanganyifu
kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye
kuujua?
Hapa tunaonywa kuhusu tabia za moyo.
Luka 6:45 Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo
mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa
kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.
Moyoni hujaa vitu ambavyo ndivyo huwa vinaamua au vinaonesha mshindi
kati ya mwili na Roho wa Mungu, kama Roho wa Mungu akikaa kwa wingi ndani yako,
moyo wako huwa ni ghala yake ya kuhifadhia mambo mema, humo huwekwa silaha na
chakula cha kuendelea kuiimarisha roho yako na kuudhoofisha mwili, lakini vivyo
hivyo kinyume chake, Mwili ukishinda basi huutawala mwili na roho yako na
kuweka chakula cha hizo roho chafu na kila aina ya kazi za uasi ndani ya moyo,
ni katika hali kama hiyo ambapo mwandishi anaandika hapa kuwa usiuache moyo
bila kuujaza mambo mema maana huwa unakuwa mdanganyifu sana katika mambo yake.
Kile kitakachoujaza moyo wako ndicho kitakachokupa ushindi katika maisha
unayotaka kuyaishi ikiwa hasa ni ya rohoni, ukiujaza moyo wako masengenyo wewe
utakuwa ni wa masengenyo tu, ukiujaza tamaa wewe utakuwa ni wa tamaa tu. Ndiyo
maana Daudi alisema kuwa moyoni mwangu nimeliweka neno lako ili nisikutende
dhambi ambapo akiisha kuliweka neno la Mungu ndani yake kwa wingi, badala ya
kuwa na mambo mengine mabaya ndani yake anakuwa na maneno ya uzima
yanayomuelekeza kutenda mema na kumuishia Mungu siku zote.
Mithali 4:23
Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
Tunaonywa
hapa kuwa moyoni ndiko kutokako chemchemi za uzima, utakachoweka moyoni mwako
ndicho hasa kitakachoamua kama wewe ni wa uzima au ni wa mauti, chunga sana
ukiwekacho moyoni, ama hakika moyo ni kama ikulu ya Mungu, ndiyo makao makuu ya
Mungu pindi ajapo ndani yake, Roho huwa ni mapokezi ya yule Mungu anayetakiwa
kuabudiwa na akiisha kupokewa, mambo yake na matendo yake na mwongozo wake
huenda kuhifadhiwa moyoni na ni kutoka pale moyoni ndipo mambo hayo huchukuliwa
na kuwekwa kwenye matendo. Kwa mfano, roho wa uzinzi humuingia mtu, akiisha
kumuingia huweka mawazo mabaya katika moyo wa huyu mtu na huyu mtu huanza kuwaza
uzinzi, akiisha kuiva katika hayo mawazo, moyo wake ukiisha kujazwa mawazo
mabaya, basi huyu mtu atakachoongea, atakachofanya na atakachofikiria itakuwa
ni uzinzi tu, maneno yote yatakuwa yanaendana na uzinzi na matendo yote hata
yasiyofungamana na uzinzi atayapeleka kwenye uzinzi. Ndiyo maana mawazo ya watu
walio wengi huwa yanapeleka maongezi mengi kwenye uzinzi, akimuona msichana
mawazo yake yanapita na yule msichana kwenye uzinzi kwanza kabla ya kuanza
kuwaza mambo mengine, hiyo ni tofauti na mtakatifu anavyotakiwa kuwaza, maana
siku zote kila nikimuona mtu natakiwa kuwaza kwanza kabla ya yote kama
amempokea Kristo au la, na kama la nitafanyaje ili ampokee, haleluya! Moyo,
ndiye mwanadamu anayetafutwa na hizi serikali mbili: Mungu na Ibilisi, Mungu
asingejivunia Ayubu kama moyo wa Ayubu ungekuwa mbali naye, au ungekuwa
unahifadhi vitu tofauti na Mungu. Mungu hakuwa anajivuna kwa jinsi
alivyombariki Ayubu, hakujivunia moyo wa Ayubu, hakujivunia umaarufu wake
isipokuwa alijivunia unyofu wa moyo wake! Tazama anavyosema
Ayubu 1:8
Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa
kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye
kumcha Mungu na kuepukana na uovu.
Hoja
kubwa anayojivunia Mungu juu ya Ayubu siyo mali, bali ni unyofu na unyenyekevu
wa Ayubu ambaye alikuwa ana “mcha Mungu na kuepukana
na uovu.” Ukiangalia swala hili ndilo alilolisema Daudi likiwa ndilo lengo hasa
la kuliweka neno la Mungu kwa wingi ndani yake- “nisije nikakutenda dhambi” kwa
hiyo tunajiridhisha kuwa moyo wa Ayubu ulijaa utakatifu na mawazo mema ya Mungu
na neno lake; ndiyo maana hata shetani aliporuhusiwa kupiga vitu vyote vya
Ayubu, bado Ayubu alibaki kuwa mwaminifu kwa Mungu wake kwani moyo wake ulikuwa
umeambatana na Mungu na siyo na vitu. Angalia sana moyo wako umeambatana na
vitu gani, maana kwa kila unayemtumikia kati ya Mungu au shetani, moyo ndiyo
unatakiwa kuwa makao makuu na hazina kuu ya ufalme husika; Mungu aliwachukia
waisraeli siyo kwa kutokwenda kanisani, bali alisema ingawa wanakuja kanisani
na kunitolea sadaka, siwakubali kwani hawa hunikubali kwa vinywa vyao tu lakini
mioyo yao iko mbali nami.
Isaiah 29:13-14
“Bwana
akanena, Kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali
mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya
wanadamu waliyofundishwa;
kwa sababu hiyo mimi nitafanya
tena kazi ya ajabu kati ya watu hawa, kazi ya ajabu na mwujiza; na akili za
watu wao wenye akili zitapotea, na ufahamu wa wenye busara wao utafichwa.”
Unaona hapa? Mungu hagombani na watu kwa sababu hawamkaribii, bali
wanamkaribia huku mioyo yao iko mbali nao! Kwa hivyo moyo ni ikulu, Mungu
akitaka kumtawala mwanadamu anamtaka mwanadamu ampe moyo wake ili apate uhalali
wa kuyaongoza maisha ya mtu huyo, na shetani vilevile atapata uhalali wa
kuyakalia maisha yako ikiwa utampa moyo wako. Maisha ya mtu na Mungu
yanafananishwa na maisha ya mtu na mpenzi wake, au maisha ya Kristo na Kanisa
yanafananishwa na maisha ya mtu na mwenzi wake. Mtu akimpenda mwenzi wake humpa
moyo wake na mtu kama huyo yuko tayari kufanya lolote ili tu asimpoteze mwenzi
wake, ni hatari kama mtu huyo akiwa amempa mwenzi wake moyo halafu yeye
hajachukua moyo wa mwenzie, ndipo unapokutana na mapenzi ya kulia kila siku kwani
mwanaume huyu aliyempa binti yule moyo masikini anajitahidi kufanya kila kitu
ili msichana yule ampende lakini wapi! Ndiyo maana watu hufikia hata maamuzi ya
kujinyonga kwa sababu kiukweli amekabidhi moyo kwa mwenziwe kwa hiyo yule
mwenzi anamuendesha kama anavyotaka maana anakuwa anajua kuwa moyo wako anao
sasa anautumia kukuendesha kama mtu abadilishavyo chaneli kwenye televisheni!
Usitoe moyo wako kwa watu ambao hawako tayari kukupa mioyo yao, utaumia! Acha
Mungu akuongoze na umpe moyo wako ili uwe salama milele na akuponye na
kukuongoza usikutane na waibao mioyo ya watu bila kutoa ya kwao. Kwenye
mahusiano tunatakiwa kubadilishana mioyo siyo mmoja achukue moyo wa mwenzie
halafu wa kwake abaki nao, ni hatariii! Pole wewe uliyekumbwa na hayo, nenda mbele
za Mungu umuombe akurudishie moyo wako ulioibiwa! Subiri nikwambie kitu, kwenye
mahusiano ni mioyo tu ndiyo inayohusika, sasa utakuta mtumishi kabla ya kuwa na
mwenzi alikuwa saa zote anatafakari neno sasa tangu amempata yule shemeji
yangu, sweet heart, amemjaza moyoni hata nafasi ya kuimba pambio na kusoma
biblia hana, akienda huku anamuwaza yeye, akirudi kwa rafiki zake anamuongelea
yeye, akipiga simu anaongea na yeye, akiandika meseji anamuandikia yeye, akilia
anamlilia yeye, akinunua zawadi anamnunulia yeye, akicheka kachekeshwa na yeye,
akilia kalizwa na yeye, akiumia hapoi hadi apewe pole na yeye, akilizwa na
mwingine hanyamazi hadi anyamazishwe na yeye. Akikatazwa jambo haachi mpaka
akatazwe na yeye! Kwenda kanisani mpaka asukumwe au asindikizwe na yeye! Sasa
mtu kama huyu akiachwa kwanini asinywe sumu jamani? Sasa unajiuliza hapa nataka
kusema nini, nasema uwe na kiasi na kukesha-naye Bwana atakupa taji ya uzima.
Mwenye masikio ya kusikia na asikie. Unasikia wewe kijana, hatujaanza leo kuwa
na wapenzi na wala sisemi kuwa kuwa na wapenzi ni vibaya la! Ninachosema ni
kuwa kuutiisha mwili ni pamoja na kuupunguzia na kuudhibiti pale ambapo
unaonekana kuvuka mipaka, kwani unafikiri kwanini watu wanazini na ndugu zao?
Ni kwasababu mwili usipodhibitiwa huendelea mbele na kufanya mambo yasiyofaa na
hivyo mwenye mwili asipouzuia, mwishowe atafanana na Ibilisi. Unataka
kumpendeza Mungu, basi funga, omba, jitakase soma neno, sasa wewe unayeshinda
na mwenzi wako hayo utayafanya saa ngapi? Watu kama wewe ndo wale ambao
wakiisha kuoana wanataka wawe wanashinda ndani na wapenzi wao wakitazamana na
kucheza usiku kucha, huwa hawakawii kushinda njaa! Muache mumeo amtafute Mungu!
Muache mchumba wako amtafute Mungu! Muache sweetheart wako amtafute Mungu!
Mkaripie pindi anapoonesha udhaifu katika kumtafuta Mungu! Au unataka kuingia
mbinguni peke yako? Haaaaaaaaah! Tunapoongelea kwa mfano suala la kufunga,
hatusemi chakula hakina maana, chakula ni afya lakini tunalazimika kufunga ili
kuiadabisha miili yetu mbele ya Mungu, hatusubiri miili kupoteza hamu ya kula
ili tufunge, tena siku nzuri ya kufunga ni ile unayojisikia kula na una njaa
tangu saa kumi na moja alfajiri! Unajua nikushirikishe jambo hapa, nimewahi
kufundisha watu kuhusu sadaka, kwa kusema kuwa unapomtolea Mungu sadaka usitoe
cha ziada bali kile ambacho kinauma. Mungu wetu siyo Mungu wa mabaki bali Mungu
wa kilicho bora! Ndiyo maana hata wewe umechagua mchumba mzuri kweli! Unaona
ee? Yaani katika ufalme wako (katika mbingu yako) hutaki kinyonge kiingie! Na
vilevile Mungu anataka the best! Kilicho bora kabisa! Sasa huyu kwa vile
alivimbiwa jana akateseka sana anataka afunge leo maana hana ‘mudi’ ya kula,
looh! Aibu! Tunafanya vitu hata tusivyojisikia kufanya kwa ajili ya Bwana kwa
sababu sisi tu watumishi wake, hata tukiwa wana tunatakiwa kufuata mfano wa
Kristo maana anasema mimi sikusema wala kufanya jambo lolote lile isipokuwa
nililoagizwa na baba, pale Getsemane unaona Yesu anasema mapenzi yako baba
yatimizwe, ina maana yeye anajisikia kutoendelea kama wewe leo unavyoweza
kujisikia kuacha kusudi la Mungu. Lakini hebu tiwa nguvu na umwambie Mungu ili
mapenzi yake katika maisha yako yatendeke kwa jina la Yesu!
No comments:
Post a Comment